RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ametangaza hali ya hatari kwa waamuzi watakaochezesha Ligi msimu ujao.
Akifunga semina ya waamuzi hao iliyokuwa ikifanyika makao makuu ya TFF, Karia amesema, msimu ujao utakuwa wa tofauti ambapo watahakikisha wanasimamia umakini.
Karia, aliyeambatana na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Nassoro Idrissa, amesema waamuzi watakaoshindwa kucheza vyemau wakibainika kwa makosa hayo, wataondolewa moja kwa moja katika majukumu hayo.
“Huu ni msimu tunaotarajia utakuwa tofauti sana, tukimaliza tutapongezana, lakini kwa wale watakaokuwa tofauti tutakuwa tumeachana nao moja kwa moja,” amesema Karia na kuongeza;
“Wala hilo sitanii, tutaachana nao moja kwa moja, ipo Kamati ya waamuzi, lakini tuna wakufunzi wetu, kuna utaratibu tutatengeneza, tuwe na ‘paneli’ ya kuwajadili waamuzi.
“Mwenyekiti (TPLB) najua wewe ndiye Mwenyekiti wa ile Kamati (Kamati ya Usimamizi wa Ligi), kama utaendelea na utaratibu kama wenzako, ie inayojadili matukio ya ligi, naomba sana waamuzi ambao mtaona wana hitilafu, nyie warudisheni katika paneli…paneli hiyo itafanya kazi yake ikishirikiana na vyombo vingine.”
Pia Karia ameongeza, kwa matukio ya msimu uliopita ya makosa ya waamuzi yalisababisha mtikisiko wa nchi kiasi cha kufikia kuitikisa serikali.
“Tumeshakuwa na mazungumzo mengi sana na serikali kuhusu hali halisi, niseme ukweli naamini uwezo mnao na mnajua vizuri kutafsiri sheria, huu mpira wetu tumeshaufikisha sehemu kubwa sana sehemu ambayo Dunia nzima inatutambua sasa, hivyo tusiwe chanzo cha kuporomoka.”