ZIKIFANYIKA kwa mara ya kwanza nchini mbio za nyika na vikwazo chini ya Mlima Meru uliopo Arusha, ni ubunifu wa aina yake utakaobeba michezo, utalii pamoja na afya ya akili na mwili.
Zaidi ya kukimbia kwa miguu, pia kulikuwapo na mbio za baiskeli na shindano la pikipiki za Enduro yote yakija na utalii wa vivutio kandokando ya Mlima Meru, mlima wa pili kwa urefu nchini Tanzania.
Mkoa wa Arusha, ambao ni kitovu cha utalii nchini uliandaa mbio za nyika na vikwazo pembezoni mwa Mlima Meru ambazo zilishirikisha zaidi ya wakimbiaji 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania, kwa mujibu wa waandaji Quality Sports Promoters.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed ambaye alikuwa ni mmoja wa washiriki, ameiambia Mwanaspoti kwamba ni mara ya kwanza kwa wao kuandaa mbio za milimani na vikwazo baada ya kuwa wameandaa mara mbili mbio za nyika kuzunguka Mlima Meru.
“Ni mbio ngumu na zina vikwazo vingi, mimi nilipotea msituni wakati nikishiriki,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kwa mujibu wa waandaaji, mbio za msituni na vikwazo zimepigwa katika Hifadhi ya Msitu wa Meru-Usa ambapo kabla ya kupigwa kwa mbio hizo, washiriki walikuwa wamefanya kambi ya usiku kucha (pikiniki) katika msitu huo, kwa mujibu wa mmoja wa waandaaji, Xavier Chuwa.
Aliongeza kwa kusema, wataalamu wa mbio za msituni kutoka nchi za Ulaya pia walishirikishwa katika kuandaa njia na taratibu za kufuatwa kwa washiriki na waandaaji wa mbio hizo.
“Mbio za vikwazo na mlimani ni maarufu sana katika nchi za Ulaya hasa Uswisi na sisi tumeamua kuuleta hapa ili uwe ni sehemu ya utalii,†alisema Chuwa.
Akieendelea, alisema kuna uwezekano mkubwa kuwapata washiriki wengi wa kigeni katika michuano ijayo ya mbio za msituni na vikwazo.
Mbio za msituni na vikwazo ni aina ya mbio ndefu kama marathoni au decathlon ambapo hujumuisha mbio ndefu, mbio za baiskeli, mbio za pikipiki za Enduro, matembezi ya msituni na yoga.