Melo alaani ofisi za JamiiForums kuvamiwa, Msigwa amjibu asema…

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo amesema kuna uvamizi usio rafiki umefanyika katika ofisi zao zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na amedai kuwa wavamizi walikuwa wakimtafuta yeye, huku Serikali ikisema haukuwa uvamizi bali ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano na anatakiwa kutoa ushirikiano na asizue taharuki katika jamii.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram leo Ijumaa Septemba 5, 2025  Melo amesema: “Kuna uvamizi usio rafiki uliofanyika muda siyo mrefu katika ofisi za JamiiForums, Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakinitafuta mimi. Nalaani vitendo kama hivi, ila umma utaujua ukweli hivi karibuni.”

Hata hivyo, hakufafanua ni kina nani waliohusika na uvamizi huo, wala sababu zilizowafanya kuingia katika ofisi hizo.

Hata hivyo, jitihada za Mwananchi kumpata Melo kuzungumzia kwa undani sakata hilo zinaendelea kwani, hakuweza kupatikana hata kupitia simu yake ya kiganjani, lakini Mwananchi inaendelea kumtafuta ili kupata ufafanuzi zaidi.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake wa X amesema hakuna uvamizi uliofanyika katika ofisi za Jamii Forums.

“Kilichotokea ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano kati ya mamlaka za Serikali na wadau wake ambapo leo maofisa wa Serikali walikwenda kuwasilisha barua ya wito kwa Jamii Forums. Ndugu Maxence Melo usilete taharuki isiyo na sababu za msingi, toa ushirikiano,” ameandika Msigwa.

JamiiForums ni moja ya majukwaa makubwa ya mtandaoni nchini Tanzania yanayojulikana kwa mijadala ya masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.