Mnigeria arithi mikoba ya Assinki Singida Black Stars

BAADA ya Singida Black Stars kumtoa kwa mkopo aliyekuwa beki wa timu hiyo Mghana, Frank Assinki, uongozi wa kikosi hicho tayari umekamilisha usajili wa Mnigeria Victor Chukwuemeka Collins, ili kurithi mikoba yake kwa mkataba wa miaka miwili.

Collins aliyezaliwa Novemba 2, 2024, katika mji mkuu wa jimbo la Enugu, Nigeria, amekamilisha usajili huo kwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine mmoja, akijiunga na kikosi hicho akitokea, Nasarawa United FC.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Collins ni miongoni mwa mabeki bora wa kati wanaoweza kurithi nafasi ya Assinki, huku akitazamiwa kutengeneza pacha kali eneo hilo na nyota wenzake raia wa Ivory Coast, Anthony Tra Bi Tra. “Moja ya pendekezo la kocha, Miguel Gamondi lilikuwa ni kupata beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto kwa ufasaha kwa sababu Tra Bi anatumia kulia, baada ya machaguo mengi tukafikia uamuzi wa kumchukua, Collins,” kilisema chanzo hicho.

Collins aliyecheza Nasarawa United na Remo Stars FC zote za kwao Nigeria, amewahi kucheza pia Amanat Baghdad SC ya Iraq, akitazamiwa kuongeza uzoefu kikosini humo, kitakachoshiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026.

Beki huyo anayetazamiwa kutengeneza pacha kali na Tra Bi, anapaswa kupambana zaidi ili kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha kocha, Miguel Gamondi kwa sababu ya ushindani uliopo, huku akiwa pia nahodha wa timu hiyo, Kennedy Juma.