Mtibwa kuchomoa wawili Singida Black Stars

MABOSI wa Mtibwa Sugar wanafanya mazungumzo na uongozi wa Singida Black Stars ili kupata saini ya nyota wawili wa timu hiyo kwa mkopo akiwamo, beki wa kushoto Mghana, Ibrahim Imoro na kiungo mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Serge Pokou.

Imoro aliyejiunga na timu hiyo Julai 1, 2024, akitokea Al-Hilal Omdurman ya Sudan, awali alikuwa anawindwa na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, ingawa dili hilo kuna uwezekano wa kufeli, huku Mtibwa Sugar ikiingilia kati kumpata.

Kwa upande wa Pokou aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea pia Al-Hilal Omdurman ya Sudan na kukitumikia kikosi hicho kwa miezi sita, inaelezwa atatolewa ili kubalansi idadi ya nyota 12 wa kigeni wanaohitajika.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Imoro aliyewahi kuzichezea Bolga All Stars, Karela United na Asante Kotoko zote za kwao Ghana, inadaiwa atakamilisha usajili huo wa kujiunga na Mtibwa, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja.

“Usajili wa safari hii tutabadilisha baadhi ya mifumo tuliyojiwekea, utakumbuka tuliachana na falsafa za kusajili tena wachezaji wakigeni, ila msimu huu tumerudisha hilo ili kutengeneza kikosi bora na cha ushindani,” kilisema chanzo hicho.

Nyota wapya wa kikosi hicho ni Datius Peter, Omary Buzungu waliotoka Kagera Sugar, Ezekia Mwashilindi, Vedastus Mwihambi (TZ Prisons), Kassim Shaibu ‘Mayele’ (TMA FC) na aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Ismail Aidan Mhesa aliyetoka Geita Gold.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2023-24, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara msimu wa 2024-25 ikiwa na pointi zake 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea baada ya kushuka daraja 2022-2023.