Nafasi ya huduma rasmi za kifedha katika Dira 2050

Dar es Salaam. Wananchi wametakiwa kutumia mifumo rasmi ya kifedha ikiwemo huduma za benki ili kuiwezesha Tanzania kutimiza malengo ya kuwa taifa lenye uchumi jumuishi na shindani ifikapo 2050.

Hayo yalielezwa jana Septemba 04, 2025 wakati wa kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) likilenga kuangazia fursa na changamoto za sekta hiyo katika utoaji wa huduma za kifedha nchini.

Mwenyekiti wa TBA, Theobald Sabi alisema wananchi wasipounganishwa na mifumo hii, kutakuwa na kundi kubwa lisiloshiriki ipasavyo katika maendeleo ya taifa

Ili kufikia azma hiyo, Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayehusika na usimamizi sekta ya fedha, Sadat Mussa alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali na sera rafiki na kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi hadi vijijini.

Alisema kama ambavyo dira inaelekeza kwamba kufikia 2050 Tanzania iwe na uchumi jumuishi, Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kifedha zikiwemo zinazotolewa na benki.

“Tunaamini sekta ya kibenki ina mchango mkubwa katika ukuzaji uchumi, tunafahamu si Watanzania wote wamefikiwa na huduma za kibenki lakini zipo taasisi ambazo zinawaunganisha na mfumo wa kibenki.

“Sisi kama wasimamizi, tutaendelea kutoa motisha mbalimbali kuhakikisha benki zinasogeza huduma zake kwa wananchi na huduma hizo ziwe kwa gharama nafuu ili kuwavutia wengi kuzitumia,” alisema.

Kwa msingi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Tuse Joune alizitaka taasisi za fedha kuwekeza zaidi katika elimu ya kifedha ili wananchi waelewe matumizi sahihi ya huduma hizo.

“Bado kuna ile dhana kwamba huduma za kifedha zina gharama kubwa, hayo mambo hayako kwa sasa kulingana na maboresho ya miongozo yaliyofanyika, huduma hizi kwa sasa ni nafuu. Kilichobaki kwa sasa ni sisi watoa huduma kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za kifedha.

“Nafurahi sasa hivi benki nyingi zina huduma ambazo zinapatikana kwa urahisi kwenye simu, hii inamfanya mtu asitumie muda mrefu kuitafuta benki anapata huduma zote muhimu kwenye simu.