NEMC YAJA NA USAFI KAMPENI 2025

::::::::

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezindua kampeni mpya ya usafi iitwayo “NEMC Usafi Campaign 2025” yenye lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika usafi wa mazingira na kuhakikisha nchi inakuwa safi, salama na yenye afya kwa wote.

Kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, mamlaka za mikoa na Halmashauri, Taasisi binafsi, Asasi zisizo za kiserikali na wananchi, inalenga kuibua mabadiliko ya tabia na kukuza uwajibikaji wa pamoja katika kudhibiti ongezeko la uchafuzi wa mazingira, hasa taka ngumu na plastiki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na utekelezajinwa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu alisema kwa sasa Tanzania inazalisha takriban tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka kwa mwaka, huku wastani wa uzalishaji taka kwa mtu mmoja ukiwa kati ya kilo 0.66 hadi 0.95 kwa siku. Hali hii inahitaji jitihada za dhati kutoka kwa kila mtanzania.

“Kampeni hii inalenga kuondoa dhana kuwa usafi ni jukumu la serikali pekee. Kila mtu anapaswa kushiriki, kwa kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inamtaka kila mtu kuwa mdau na mlinzi wa mazingira,” alisema Baruti.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo imeweka hifadhi ya mazingira kuwa moja ya mihimili ya maendeleo endelevu. Kupitia kampeni hii, taka zitatazamwa kama fursa ya ajira kupitia miradi ya kijani, vijana na wanawake watawezeshwa kupitia mafunzo ya ujasiriamali wa mazingira, huku upandaji miti ukihamasishwa kwa nguvu zote.

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika chini ya kampeni hiyo ni pamoja na operesheni za usafi, mafunzo ya elimu ya mazingira, mashindano ya usafi kwa shule na kata, uanzishaji wa bustani za kijani, maonesho ya bidhaa rafiki kwa mazingira, pamoja na uanzishwaji wa klabu za mazingira katika shule zote za msingi na sekondari ifikapo Juni 2026.