Nyongeza ya pensheni inaposababisha kizungumkuti kwa wastaafu

Mstaafu wetu anadhani kuwa litakuwa jambo jema kwa Seri-kali na mifuko inayohusika kuliweka sawa hili la nyongeza ya pensheni ya wastaafu waliokuwa wakipata mshahara wa kima cha chini. Maana sasa linaishia kuwapa wastaafu kimuhemuhe, kama siyo kuwabananga na kuwabagaza.

Tukumbuke kuwa miezi 11 iliyopita, Oktoba mwaka jana, Seri-kali hatimaye iliamua kuwapa wastaafu wa kima cha chini cha mshahara nyongeza ya pensheni ya Shilingi elfu hamsini, baada ya kutofanya hivyo kwa miaka 20 ya kilio na kusaga meno kwa wastaafu waliokuwa wakipokea Shilingi laki moja na elfu tano. Ni Mungu tu ajuaye walivyoweza kuishi kimiujiza kwa hela hiyo kwa mwezi kwa miaka 20.

Hatimaye, rudia, hatimaye Serikali ikakubali kuwaongeza Shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yao na kumfanya mstaafu apokee pensheni ya Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, katika kile Seri-kali ilichosema ni kuboresha hali ngumu iliyokuwa ikimkabili mstaafu, anayeomba mumkumbushe maana halisi ya neno “kuboresha.”

Mei mwaka huu, Seri-kali ikaboresha tena pensheni ya wastaafu wa Idara ya Hazina kwa Shilingi laki moja na elfu hamsini na kuwafanya wastaafu wa idara hiyo kuwa kweli na “hazina” kwenye mifuko yao kwa kupokea sasa pensheni ya Shilingi laki tatu kwa mwezi, huku sisi wengine tukiwa tumegota kwenye Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi.

Tukajiuliza tofauti iliyokuwapo kati ya wastaafu wa Hazina na wastaafu tuliopo huku ‘uswahilini’ iliyowafanya wao waongezwe Shilingi laki moja na nusu kwenye pensheni yao ya Shilingi laki moja na nusu na kuwafanya wapate Shilingi laki tatu kwa mwezi, huku sisi wa ‘uswahilini’ tuliokuwa tukipata Shilingi laki moja na elfu tano tukaongezwa Shilingi elfu hamsini tu na kuishia kupata Shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi! Definitely, something was not right somewhere, Kisambaa kwa msisitizo.

Hata ile ya kwamba wote ilibidi tutakiwe kusubiri miezi mitatu kwanza, sisi Oktoba hadi Januari na Hazina Mei hadi Julai, ndipo nyongeza hiyo iingie mifukoni mwetu, hilo halikutufariji sana.

Tuliishia kujiona kama tuko kwenye lile ‘shamba la wanyama’ la mtunzi George Orwell, aliposema kuwa wanyama (tamka binadamu) wote ni sawa, lakini kuna wengine wako sawa zaidi kuliko wengine! Hapa Bongo zamani tulikwishajua kwamba ni kweli.

Ikaelekea kuwa imekuwa ‘pati gazeti’ kwa baadhi ya wastaafu ambao wamewasiliana na mstaafu mwenzao huyu na kumueleza kuwa wao hawajaiona hiyo nyongeza ya Shilingi elfu hamsini iliyotangazwa na Seri-kali kwamba ni ya kuboresha maisha yao, kwa Shilingi elfu hamsini, ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya ustaafu inayowakabili.

Kwamba bado wanapokea ‘laki si pesa’ kama walivyofanya kwa miaka 20 iliyopita, kiasi cha kuingiwa na woga kwamba Mungu atachoka sasa kuwafanya waishi kimiujiza kwa miaka 20 kwa pensheni ya Shilingi laki moja na elfu tano, na akaamua yaishe tu Kinondoni!

Mstaafu anaifahamisha Seri-kali na vibubu vya akiba ya wastaafu vinavyohusika kwamba kuna wastaafu kadhaa ambao mpaka leo hii nyongeza ya pensheni iliyotamkwa na Seri-kali bado haijaingia kwenye mifuko yao, na bado wanaishi kimiujiza kwa pensheni ya ‘laki si pesa!’

Mstaafu anaiomba Seri-kali na vibubu vinavyohusika kuchukua hatua za haraka kuwasaidia wastaafu hawa kupata wanachostahili. Maana ana hakika kuwa wale wastaafu wanaopokea pensheni iliyo sawa na mshahara wa walimu ama walinzi wetu hawaambiwi wasubiri miezi mitatu ili nyongeza ya mishahara yao iingie mifukoni mwao!