Timu ya mpira wa kikapu ya Risasi iliifunga Kahama Sixers kwa pointi 64-61, katika fainali ya Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Shinyanga iliyofanyika kwenye Uwanja wa Pope Leone XV uliopo Kahama.
Ushindi umeifanya timu hiyo itwae ubingwa kwa matokeo ya jumla ya michezo 2-1, ambapo katika fainali ya kwanza Kahama Sixers ilishinda kwa pointi 97-77, fainali ya pili na ya tatu Risasi ikashinda kwa pointi 72-67, 64-61.
Katika fainali ya tatu Risasi iliongoza kwa kufunga pointi 11-10, 26-21, 12-14, 15-16.
Katika mchezo huo, Venace Mangula kutoka timu ya Risasi alifunga pointi 12, akifuatiwa na Nuhu Makang’a aliyefunga pia pointi 12, huku Julius George kutoka Kahama Sixers akifunga pointi 15.
Timu ya Kahama Sixers ilitinga fainali ni baada ya kuifunga timu ya Veta kwa michezo 2-0, huku timu ya Risasi ikiifunga B4 Mwadui kwa michezo 2-0.
Katika fainali iliyofanyika mwaka jana, timu ya Kahama Sixers iliishinda timu ya Risasi kwa michezo 2-1.
Kamishina wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya Mkoa wa Shinyanga, George Simba, amesema fainali ya Ligi ya mwaka huu ilikuwa ni ya ushindani mkubwa.
Akizungumzia kuhusiana na timu za wanawake, alisema mwakani timu za wanawake zitashiriki Ligi ya Mkoa wa Shinyanga.