Simbu, Gisemo kubeba mioyo ya Watanzania Tokyo

MATUMAINI ya Tanzania kuongeza medali ya tatu katika historia ya mashindano ya dunia ya riadha yapo mikononi mwa wanariadha wawili Aphonce Simbu na Josephat Gisemo watakaoshiriki kuanzia Septemba 13, mwaka huu, jijini Tokyo, Japan.

Awali, Tanzania ilitarajia kupeperusha bendera kwa wanariadha wanne, lakini mipango hiyo ikayumba baada ya bingwa wa marathoni wa Wanawake, Magdalena Shauri na Failuna Abdi Matanga, kushindwa kushiriki kutokana na kuchelewa kupima vipimo vya jinsia vinavyohitajika na Shirikisho la Riadha la Dunia (WA).

Simbu anarudi Tokyo akiwa na kumbukumbu ya kumaliza nafasi ya saba kwenye Olimpiki 2020 kwa muda wa saa 2:11:35, lakini zaidi akiwa na historia ya kutwaa medali ya shaba kwenye mashindano ya dunia ya mwaka 2017 London, Uingereza akitumia 2:09:51.

Nyota huyo kutoka timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), anakwenda Japan na rekodi ya 2:04:38 kutoka Valencia marathon mwaka jana pia nafasi ya pili Boston Marathon kwa 2:05:04 Aprili, mwaka huu.

Gisemo wa Jeshi la Polisi anakwenda Tokyo kwa mara ya kwanza akiwa anabebwa na muda wa saa 2:10:23 alioupata Geneva Marathon nchini Uswisi mwaka jana, na anachukuliwa kama kadi mpya ya ushindi kwa Tanzania.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Stephen Akhwari amesema mashindano hayo ni sawa na Kombe la Dunia la Soka kwa sababu yanakusanya wakimbiaji bora duniani, lakini anaamini Simbu na Gisemo wanaweza kuwapa furaha nyingine Watanzania.

Akhwari aliyewahi kushiriki mashindano matano ya dunia kati ya 2001 hadi 2009 katika mbio za mita 5000 na 10,000, ameongeza kuwa maandalizi ya mwisho ya wanariadha hao ni lazima yazingatie umakini.

“Huu sio muda wa mazoezi magumu, huu ni muda wa kupumzika na kujiweka sawa kisaikolojia kabla ya vita halisi”, amesema Akhwari.

Mwanariadha wa zamani wa Kimataifa, Zakia Mrisho, ambaye ameshiriki mbio hizo kuanzia 2003 hadi 2011 akikimbia mita 5000 naye ameweka bayana matumaini yake kwa nyota hao akiamini kutokana na maandalizi wanayoendelea kufanya watarudi na medali.

“Naamini Simbu na Gisemo wanaweza kutupa historia mpya ukizingatia Simbu alitupa medali ya shaba mwaka 2017,” amesema Mrisho.

Tanzania inajivunia medali mbili pekee tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 1983 Helsinki Finland ikiwakilishwa na baadhi ya nyota akiwemo Gidamis Shahanga, Zakaria Barie na Abraham Mikumi.

Medali ya kwanza ni ya fedha ambayo ilipatikana mwaka 2005 hukohuko Helsinki, Finland kupitia kwa Christopher Isengwe ambaye alimaliza wa pili mbio ndefu akitumia saa 2:10:21. Nyingine ni ya shaba kutoka kwa Alphonce Simbu 2017 London, Uingereza akitumia 2:09:51.