KIKOSI cha Simba kinaendelea na maandalizi ya tamasha la Simba na mechi za kufungulia msimu mpya wa 2025-26, lakini kuna mastaa wawili wapya bado hawajaanza kazi na kikosi hicho, japo tayari wameshatambulishwa na mmoja kati ya hao ni beki aliyemshtua kocha wa zamani wa Yanga.
Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo Misri akiendelea na majukumu yake, amefichua kuwa Simba imepata beki kwa kumnyakua Wilson Nangu, akifunguka kuwa, kama jamaa akijiongeza kidogo tu anapindua meza kwa wekundu hao kwa namna alivyo mtu sana katika eneo la ulinzi.
Ipo hivi. Nangu sambamba na kipa Yakoub Suleiman wote bado hawajaanza rasmi kazi licha ya wote kutambulishwa juzi wakitokea JKT Tanzania, ambapo Simba ililazimika kuvunja benki ili kuinunua mikataba waliyokuwa nayo.
Hata hivyo, kocha wa zamani wa Yanga, Miloud Hamdi akiwa Ismailia Misri, amesema alimuona Nangu wakati Yanga ikicheza dhidi ya JKT kisha akakubali ubora alionao na alikuwa akimpigia hesabu kumvuta Jangwani.
Hamdi ambaye timu yake ya Ismailia inapambana kutafuta ushindi wa kwanza katika Ligi ya Misri, alisema Nangu ni beki mzuri ambaye kama akijipanga anaweza kufanya makubwa akiwa na Simba.
Alisema beki huyo alimfurahisha alipowazuia washambuliaji wake wa zamani Yanga kwa hesabu nzuri ambapo anaamini kama ataendeleza kiwango kile, anaweza kupangua safu ya ulinzi ya Simba.
“Namkumbuka yule beki alikuwa anavaa jezi namba 21 (Nangu) ni beki mzuri nadhani Simba imepata beki mzuri, nilimuona nilipokutana naye mara ya kwanza kwenye ligi (dhidi ya Yanga) alicheza vizuri sana ile mechi,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Tulipokutana naye mara ya pili kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) tukashinda lakini bado alicheza vizuri, anacheza kwa hesabu sana hampi nafasi mshambuliaji kuamua kitu na hiki ndicho ambacho beki anatakiwa kukifanya.
“Kama atakwenda kuendeleza kile alichofanya anaweza kufanya vizuri, nadhani wapinzani wangu wa zamani wamepata chaguo zuri.”
Kocha huyo alifafanua zaidi kwa kusema kama angesalia Yanga, alikuwa na hesabu za kumchukua beki huyo pamoja na beki mwingine wa pembeni wa timu hiyo ambao alikubali ubora wao.
“Ukiacha huyo namba 21 (Nangu) pale kulikuwa na beki mmoja wa pembeni, naye nilimkubali sana, kama ningebaki Yanga nilikuwa nataka kuwachukua hao wawili, ila ukweli kabisa Simba ina kila sababu ya kujivunia kumbeba beki huyo wa kati.”
Nangu aliyeitumikia JKT msimu uliopita akitokea TMA Stars iliyopo Ligi ya Championship, amesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu sambamba na Yakoub, lakini wameshindwa kuungana na wenzao kambini kwa vile wapo na timu ya taifa inayocheza leo ugenini dhidi ya Congo.
Nyota hao wawili walioibeba JKT na kumaliza nafasi ya sita katika msimu wa Ligi Kuu iliyopita, kabla ya hapo walikuwa na Stars katika michuano ya CHAN 2024 ambapo timu hiyo ilikwamia robo fainali ikipoteza kwa bao 1-0 mikononi mwa Morocco iliyoenda kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.