Straika Majimaji ageukia udiwani | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa zamani Majimaji, Stand United, Alliance na Singida United, Six Mwasekaga amegeukia siasa akijitosa kuwania udiwani kupitia chama cha ACT Wazalendo katika Kata ya Mbugani, wilayani Kyela, mkoa wa Mbeya.

Mwasekaga aliliambia Mwanaspoti kwa sasa hachezi mpira wa ushindani na ameona ana nafasi ya kufanya kitu katika jamii kupitia siasa.

“Kitu kikubwa kilichonishawishi ni dhamira ya kuwasimamia wazee, kina mama wajane kupata haki zao za msingi yakiwepo matibabu kupitia bima za afya, hilo litafanya wafurahie maisha ya uzee wao,” alisema Mwasekaga na kuongeza;

“Jambo jingine nikifanikiwa natamani kata yetu iwe na huduma za maji hata ya kuchimba visima ili kuwatua wanawake ndoo vichwani pia natamani kuanzisha soko la jioni kwa wafanyabiashara wadogo maeneo ya mwisho wa lami, ili wasifanye kando ya barabara jambo ambalo litawaepusha na hatari za ajali.”

Alisisitiza wakati anacheza soka la ushindani alikuwa anasapotiwa na jamii, hivyo anaona ni fursa sahihi ya kuwatumikia wao kwa sasa: “Tangu zamani napenda kusaidia jamii nje na camera, naamini Mungu anapokupa kidogo unagawana na wenzako.”

Mwaka 2023 Majimaji iliposhindwa kulipa pesa ya hoteli jijini Dar es Salaam Mwasekaga aliwachukua wachezaji 21 na kwenda kukaa nao nyumbani kwake Kigamboni kwa siku nne na benchi la ufundi alilipia sehemu ya kulala wageni.

“Baada ya kufukuzwa katika hoteli ambayo walifikia, Erasto Nyoni akiwa Simba alilipa deni, mimi nikawachukua kwenda kukaa nao kwangu, kifupi siyo kila jambo ninalofanya katika jamii nitalitangaza, hivyo nia yangu kubwa ni kuona jamii inayonizunguka haipati shida,” alisema nyota aliyewahi pia kucheza Tanzania Prisons, Polisi Moro (sasa Polisi Tanzania) na AFC Arusha.