Taifa Stars mzigoni tena | Mwanaspoti

BAADA ya kumaliza kazi kwenye Fainali za CHAN 2024 zilizoandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars usiku wa leo kitakuwa kibaruani ugenini katika mechi ya kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia za 2026.

Tanzania itavaana na Congo Brazzaville kwenye Uwanja wa Alphonce Massamba-Debat ikiwa ni mechi ya Kundi E itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Tanzania kwa sasa ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi tisa, kupitia mechi tano, nyuma ya Morocco yenye alama 15 iliyopo nyumbani kuikaribisha Niger kuanza saa 4:00 usiku.

Stars chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ ilifika robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda tayari ipo jijini Brazzaville tayari kwa pambano hilo ikisaka pointi tatu muhimu zitakazofufua matumaini ya kucheza fainali hizo.

Hili ni pambano la pili kwa Tanzania dhidi ya Congo katika kundi hilo, baada ya awali kupata ushindi wa mezani kutokana na wenyeji kufungiwa na FIFA na kusababisha kugawa alama za bure kwa timu nyingine za kundi hilo, ikiwamo Zambia na Niger kabla ya kufutiwa adhabu.

Ushindi wa ugenini utaifanya Stars kuendeleza rekodi tamu katika kundi hilo, kwani mechi mbili kati ya tatu ilizocheza hadi sasa imetoka na ushindi ikiifumua Niger na Zambia kwa bao 1-0, japo ile dhidi ya Morocco ilicharazwa mabao 2-0, ukiacha ushindi wa mezanni dhidi ya Congo.

Stars itaendelea kuwategemea nyota wake wa kimataifa Mbwana Samatta, Simon Msuva na Novatus Dismas sambamba na wengine wanaocheza ligi ya ndani kama kina Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ibrahim Bacca kuwabana wapinzani wao ambao hawana pointi yoyote hadi sasa baada ya kucheza mechi tano.

Awali, timu hiyo ilipoteza 4-2 mbele ya Zambia kisha kupigwa 6-0 na Morocco mbali na michezo mitatu iliyotoa pointi za dezo, ikifunga mabao mawili na kufungwa 19, kitu kinachoipa jeuri Tanzania kuamini itatoka na ushindi wa tatu ugenini mbele ya wenyeji wao hao.

Stars inayomiliki mabao matano na kufungwa manne yote yakitokana na vipigo vya nje ndani kutoka kwa Morocco, inapaswa kuwa makini dhidi ya wenyeji, kwani ni timu inayocheza kwa kasi na kufunga mabao kama ilivyoonekana katika mechi ya awali dhidi ya Zambia ugenini.

Katika mechi hiyo Congo ilipoteza 4-2, lakini iliwabana wenyeji na kufunga mabao yake katika dakika za mapema za kipindi cha kwanza kabla ya Zambia kupindua meza kipindi cha pili na kuibuka kifua mbele.

Kocha wa Stars, Hemed Morocco ametamba kwamba licha ya kwamba watakuwa ugenini, lakini anaamini watafanya vizuri katika mechi hiyo kabla ya kurejea nyumbani kumalizana na Niger, mechi itakayopigwa Septemba 9 kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.

Mechi nyingine zinazopigwa leo ni; Somalia v Guinea, Sudan Kusini v DR Congo, Kenya v Gambia, Namibia v Malawi, Benin v Zimbabwe, Djibouti v Burkina Faso, Lesotho v Afrika Kusini, Uganda v Msumbiji, Misri v Ethiopia, Ivory Coast v Burundi, Mauritania v Togo, Morocco v Niger, Senegal v Sudan.