TDS imeitibulia City FC Abuja katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano ya Tanzanite Pre-Season International baada ya leo Septemba 5, 2025 kuichapa bao 1-0.
City FC Abuja iliingia katika mchezo huo uliofanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, ikiwa tayari imefuzu nusu fainali, lakini ilihitaji kuweka heshima ambayo imetibuliwa.
TDS ambayo ilikuwa imepoteza mechi zote mbili za kwanza, ilipata bao pekee lililowapa heshima likifungwa na Amani Ruben Keah dakika ya 70.
Kabla ya kufungwa bao hilo, TDS inayofundishwa na Agrey Moris, ilitengeneza nafasi nyingi lakini eneo la mwisho halikuwa makini kuuweka mpira kwenye nyavu.
Licha ya kupoteza, City FC Abuja imefuzu nusu fainali kufuatia kukusanya pointi nne ikimaliza nafasi ya pili Kundi C ambalo kinara ni Namungo yenye pointi saba.
TDS imemaliza ya mwisho na pointi tatu sawa na JKU iliyokamata nafasi ya tatu.
Kesho Jumamosi Septemba 6, 2025, katika michuano hiyo itapigwa michezo ya hatua ya nusu fainali ambapo saa 7:00 mchana, Tabora United itakabiliana na Namungo, kisha saa 10:00 jioni ni Dodoma Jiji dhidi ya City FC Abuja.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yakiandaliwa na Fountain Gate FC, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali.
Jumla ya timu 10 zimeshiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A limeundwa na timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC ya Manyara.
Kundi B ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.