Ushindi wa Namungo kwa JKU, waibeba City FC Abuja

KITENDO cha Namungo FC kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKU katika mashindano ya Tanzanite Pre-Season Tournament si tu imeifanya timu hiyo kufuzu nusu fainali, bali pia imeibeba City FC Abuja.

Ipo hivi; Kabla ya mchezo huo wa Kundi C kuchezwa leo Septemba 5, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, Namungo ilikuwa kileleni na pointi nne sawa na City FC Abuja, wakati JKU ya tatu ikikusanya pointi tatu na TDS haikuwa na pointi.

Huo ukiwa ni mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi kwa timu hizo, maana yake ni kwamba Namungo imefikisha pointi saba ikiendelea kukaa kileleni, City FC Abuja (4), JKU (3) na TDS (0). 

Kama JKU ingeshinda, basi City FC Abuja ingelazimika kushinda mchezo wa jioni dhidi ya TDS ili kufuzu nusu fainali na kuiondisha Namungo, lakini sasa, City FC Abuja inakwenda kufunga dimba kwa heshima.

Katika mchezo huo ulioanza saa 7:00 mchana, Namungo ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Jofrey Julius dakika ya 10.

JKU ilisubiri hadi dakika za nyongeza baada ya kutimia 45, ambapo mkwaju wa faulo uliopigwa na Yakoub Amour Bakari, mpira ukajaa nyavuni licha ya kipa wa Namungo, Suleiman Abraham kujaribu kuudaka lakini ukateleza. Mapumziko Namungo 1-1 JKU.

Kipindi cha pili, Namungo ilikuja na moto, ikachukua uongozi tena dakika ya 54 pale Fabrice Ngoyi alipofunga bao kiufundi.

Dakika ya 60, Namungo ikatanua zaidi uongozi baada ya Hassan Kabunda kufanyiwa faulo nje kidogo ya boksi la JKU, ndipo Rodgers Gabriel akaitumia nafasi hiyo kufunga bao moja kwa moja.

Kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza, JKU ilipata bao lake la pili dakika za nyongeza baada ya 90 kukamilika ambapo mfungaji alikuwa
Koffy Hamza, likiwa ni bao lake la tatu kwenye michuano hii kufuatia mchezo wa kwanza kufunga mawili dhidi ya TDS.

Namungo na City FC Abuja zinaungana na Tabora United iliyokuwa ya kwanza kufuzu nusu fainali kutoka Kundi A, sambamba na Dodoma Jiji iliyomaliza kinara Kundi B.

Hata hivyo, City FC Abuja imefuzu nusu fainali ikiwa inasubiri kukamilisha ratiba kwa kucheza dhidi ya TDS unaotarajiwa kuanza saa 10:00 jioni ya leo.

Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yakiandaliwa na Fountain Gate FC, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Jumapili hii Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali. Kabla ya hapo, kesho Jumamosi Septemba 6, zitachezwa mechi za nusu fainali.

Jumla ya timu 10 zimeshiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A limeundwa timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC ya Manyara.

Kundi B ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.