‘Usikose kwenda haja kubwa kila siku’

Dodoma. Ninapata nafasi ya kusimama na kutoa pesa kwenye madirisha ya kutolea pesa kwenye benki (ATM) na maduka ya kutolea pesa.

Nikiwa maeneo hayo,  ninaona maneno yasemayo:  Hakiki pesa zako kabla hujatoka mbele ya dirisha la kupokelea pesa. 

Hii  ikanifanya nifikiri kumbe ni maneno muhimu. Ni sawa na kusema hakikisha unakagua dawa zako kabla ya kutoka duka au dirisha la dawa.

Leo ninaamua kutumia maneno hayo kukujulisha kuwa hakikisha unapata haja kubwa  kila siku. Hakikisha unajua unapata  haja ya aina gani  na kama kuna shida nyingine yoyote mwilini inayojitokeza unapopata haja.

Kukosa choo kwa wakati na kuvurugika kwa ratiba yako ya kupata haja kubwa,  kunaweza kuwa kiashiria cha magonjwa yanayoweza kuondoa maisha yako haraka, kama vile saratani ya utumbo mpana.
Wengine wanapokosa choo au kupata choo kigumu wanaweza kupata magonjwa ya njia ya haja kubwa kama vile bawasiri,  michubuko na pengine kubana kwa misuli ya njia ya haja kubwa.

Kwa Kiingereza  tunaita ‘constipation’ yaani hali ya kukosa haja kwa zaidi ya siku tatu na kuendelea, pamoja na kupata choo kigumu na kutumia nguvu kusukuma haja itoke mithili ya kunyanyua vitu vizito.

Katika kazi yangu ninaona wagonjwa wengi wenye tatizo hiki, wengine wamesema wanalazimika kutumia kijiti kutoa  kinyesi katika utupu, wengine wanajikakamua mpaka wanatoka jasho kama wako kwenye mazoezi na wengine wanasema yanatoka kama ya mbuzi tena kwa mbinde. Hili ni tatizo kwa lenyewe na dalili ya maradhi mengine.
Pamoja na hayo, wengine wameniambia kuwa wanaona damu inatoka kabla, wakati au baada ya haja kutoka.
Hii ni shida kubwa kwa wanaume na wanawake wengi, wengine wamepata hernia (mshipa wa ngiri) kwa sababu ya kujikakamua wakati wa kupata haja kubwa.
Baada ya haja wengi hujisafisha kwa maji, au karatasi laini au vyote. Tafadhali jitahidi ujue kama kuna damu au la.

 Na unapopapasa ukijisafisha jitahidi uone kama njia ya haja ina kitu chochote kilichotoka kama kinyama  kinatoka na kurudi ndani au kama kuna michubuko.

Hakikisha ratiba yako ya kwenda haja unaijua kama ni asubuhi, mchana au jioni, au vyote, ikibadilika tafadhali muone daktari aliye karibu nawe.
Pia hakikisha unafahamu ujazo, kipenyo na mzigo wa kinyesi chako, maana ikibadilika pengine utumbo mpana au puru imeanza kuwa na uvimbe unaoweza kuwa saratani.

Ili kupata haja vizuri ni muhimu kula chakula chenye nyuzinyuzi, mboga za majani, matunda na maji ya kunywa ya kutosha.

Pia fanya mazoezi kama kuruka kamba, kutembea au kukimbia.
Zingatia dalili za magonjwa ya mfumo wa chakula  pamoja na ukosefu wa haja. Hivyo kuwa makini kuhakiki kama unavyohakiki unapokuwa benki au ATM.

Ikumbukwe kuwa saratani ya utumbo ni miongoni mwa saratani tano zinazowapata watu wengi duniani bila kujali jinsi na kipato chao.

Mwandishi ni daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma Tanzania na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania.