Dar es Salaam. Dunia ya sasa inakumbwa na changamoto kubwa ya maradhi yasiyoambukiza, kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani, na magonjwa ya moyo.
Tofauti na magonjwa ya kuambukiza ambayo mara nyingi hutokana na vijidudu, vimelea au maambukizi ya moja kwa moja, magonjwa haya mengi kwa kiasi kikubwa yanatokana na mtindo wa maisha usio sahihi.
Kwa maana nyingine, kama wanavyoeleza wataalamu wa afya, ni magonjwa ya kujitakia.
Leo takwimu zinaonyesha kwa uwazi kwamba zaidi ya nusu ya wagonjwa wanaougua magonjwa haya, wangeweza kuyaepuka iwapo wangechukua hatua ndogo tu za kubadili tabia zao za kila siku kama vile namna wanavyokula, kufanya mazoezi na kujali afya kwa ujumla.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanachukua nafasi ya kwanza duniani kwa kuua watu.
Inakadiriwa kuwa watu milioni 41 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa haya sawa na asilimia 74 ya vifo vyote. Kati ya hao, zaidi ya milioni 17 hufariki kabla ya kufikisha miaka 70.
Takwimu za mwaka 2024 za Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF), zinaonyesha watu wazima milioni 589 walikuwa na kisukari, huku ikitabiriwa idadi yao kuongezeka na kufikia milioni 853 ifikapo mwaka 2050 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Vilevile, WHO inaeleza watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na shinikizo la damu, wengi wao wakiwa hawajui kabisa kama wameathirika, jambo linaloongeza hatari ya kupata kiharusi au magonjwa ya figo.
Kwa ujumla, maradhi haya yanapoteza nguvu kazi kubwa ya taifa letu, kuharibu ustawi wa familia na kusababisha gharama kubwa za matibabu, ambazo mara nyingi hushindwa kubebwa na kaya za kipato cha chini.
Nchini Tanzania, hali si ya kutia moyo. Kwa mujibu wa taarifa za WHO na Wizara ya Afya, takribani asilimia 33 ya vifo vyote nchini husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Shinikizo la damu linaathiri karibu mtu mmoja kati ya wanne, na kisukari kimekuwa kikiongezeka kwa kasi, hasa mijini.
Utafiti ujulikanao kwa jina la STEP Survey wa mwaka 2012, ulibaini kuwa takribani asilimia 26 ya Watanzania wana shinikizo la damu, na zaidi ya asilimia tisa wana kisukari.
Lakini kinachotia hofu zaidi ni kuwa watu wengi kati ya hawa hawana ufahamu juu ya hali zao. Wanaishi kwa kudhani wako salama, hadi pale wanapopatwa na mshtuko wa moyo ghafla au kupoteza maisha.
Kwa upande mwingine, mtindo wa maisha mijini umechochea tatizo hili zaidi. Vyakula vya haraka, vya kukaanga matumizi makubwa ya sukari, chumvi na mafuta, pamoja na kutofanya mazoezi, kumechangia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza.
Pia matumizi mabaya ya vilevi, uvutaji sigara, na msongo wa mawazo yanachangia kueneza magonjwa haya kwa kasi.
Sababu kuu inayoyafanya magonjwa haya yaitwe maradhi ya kujitakia, ni kuwa yanafikika kutokana na tabia za kila siku zinazoweza kuepukika.
‘’Ni lazima tujenge uelewa wa watu kuhusu tabia bora za kiafya, ikiwemo kula vyakula bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya pombe na sigara. Jamii zetu zinahitaji kupatiwa uelewa huu… ‘’ anasema Waziri wa Afya wa Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui.
Ni kweli kwamba kuna kipengele cha kurithi lakini tafiti nyingi zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya vifo vinavyotokana na magonjwa haya vina uhusiano wa moja kwa moja na maisha tunayoishi.
Maisha hayo ni pamoja na kutosoma lebo za vifungashio zinazoonyesha usalama wa viambato vya vyakula vilivyomo, lishe duni hasa ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, chumvi kupita kiasi, na kukosa mboga mboga na matunda.
Alama za onyo kwenye vifungashio
Lengo la alama au taarifa hizi ni kumrahisishia mlaji kufanya uamuzi wa haraka na sahihi kuhusu ubora wa chakula anachonunua na kula.
Taarifa hii ya lishe inayoonyesha viambata vilivyomo kwenye chakula inapaswa kuwa fupi na iwekwe kwa namna rahisi kueleweka, mara nyingi kwa kutumia alama za rangi, alama za nyota, au nembo maalum.
Magonjwa yasiyoambukiza yanachochewa zaidi na ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, sukari kupita kiasi na nishati nyingi.
Taarifa hizi zina uhusiano wa karibu na magonjwa haya kwa kuwa huonya mlaji endapo chakula kimejaa sukari, chumvi au mafuta, ambavyo ni vihatarishi vikuu vya magonjwa haya.
Ni taarifa zinazomsaidia mnunuzi. Kwa mfano, mtu akiwa dukani anaweza kuchagua soda yenye sukari kidogo au siagi yenye mafuta kidogo kwa kuangalia alama za mbele ya pakiti.
Kubwa zaidi kadri watu wanavyozidi kuelewa alama hizi, ndivyo jamii inavyopunguza ununuzi wa vyakula visivyo na afya na hivyo kupunguza mzigo wa magonjwa ya kuambukiza.
“Magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto kubwa ya karne hii… Alama za tahadhari mbele ya kifurushi ni njia madhubuti za afya ya umma zinazopaswa kutumika,’’ anasema mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu afya, Dainius Pūras.
Kutofanya mazoezi: Wengi wetu tumekuwa na maisha ya kukaa tu ofisini au nyumbani bila mazoezi ya mwili.
Ulevi na uvutaji sigara: Haya ni sababu kubwa ya magonjwa ya moyo, saratani, na shinikizo la damu.
Pia uzito uliopitiliza.Huu unachochea sana kisukari na matatizo ya mishipa ya damu.
Kwa maneno mengine, mtu akibadili mlo wake, akafanya mazoezi, akaacha pombe na sigara, akajali afya yake kwa kufanya uchunguzi mara kwa mara, kuna uwezekano mkubwa asipate magonjwa haya kabisa.
Ni ukweli usiopingika kwamba wengi wetu tunaugua maradhi ya kujitakia. Kila siku tunaona familia zikihangaika kugharamia matibabu ya muda mrefu kwa wapendwa wao walioathirika na kisukari au shinikizo la damu. Lakini kabla ya kufika huko, tungeweza kuchukua hatua rahisi za kujilinda.
Magonjwa haya hayachagui mtu; yanamkumba kijana na mzee, tajiri na maskini, wa mijini na vijijini. Lakini kinga kubwa ipo mikononi mwetu wenyewe. Tukiishi kwa mtindo bora wa maisha kwa kula vizuri, kufanya mazoezi, kuepuka ulevi na sigara, pamoja na kufanya uchunguzi wa kiafya mara kwa mara, tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa mateso haya.