SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limewateua waamuzi wa Tanzania, Ahmed Arajiga, Mohamed Mkono, Kassim Mpanga na Ramadhan Kayoko kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya ASCK ya Togo dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.
Waamuzi hao watachezesha mchezo huo uliopangwa kufanyika Septemba 21, 2025 kwenye Uwanja wa Kégué dé Lomé nchini Togo.
Huo ni mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali, kisha timu hizo zitarudiana wiki moja baadaye nchini Morocco ambapo mshindi wa jumla anafuzu hatua inayofuata katika mtoano kuwania kufuzu makundi.
Mshindi wa mechi hizo mbili, atakutana na mshindi kati ya Dadjè FC ya Benin na Al Ahli Tripoli kutoka Libya.
Hivi karibuni, Arajiga alikuwa kwenye orodha ya waamuzi wa kati waliochezesha mechi za mashindano ya CHAN 2024 yaliyofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Katika mashindano hayo, Tanzania ilikuwa na waamuzi wawili, Arajiga na Hamdani Said ambaye ni mwamuzi wa msaidizi.
Arajiga alichezesha mechi ya mwisho Kundi C kati ya Algeria dhidi ya Niger iliyochezwa Agosti 19, 2025 kwenye Uwanja wa Nyayo nchini Kenya na kumalizika kwa timu hizo bila kufungana.