NYOTA mpya wa Singida Black Stars, Clatous Chama ameanza vitu na kuibua matumaini kwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye alikosa huduma yake katika mechi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Kagame dhidi ya Ethiopian Coffee kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Baada ya mechi hiyo, Gamondi alieleza wazi kwamba walikosa mtu mwenye ubunifu ambaye angeweza kuifanya kazi kuwa nyepesi kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji kiasi cha kushindwa kutamba dhidi ya timu ambayo ilikuwa pungufu kwa zaidi ya dakika 30.
Chama ambaye amejiunga na Singida BS kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, alianza mazoezi na kikosi hicho, juzi mara baada ya kutua nchini akitokea kwao, Zambia.
Fundi huyo wa zamani wa Yanga na Simba, ameeleza furaha yake kufuatia kujiunga na timu hiyo huku akiwa na matarajio makubwa chini Gamondi ambaye aliwahi kufanya naye kazi Jangwani kabla ya kuondoka.
“Nipo tayari kwa changamoto mpya, nina furaha kujiunga na Singida BS, jukumu langu kwa sasa ni kusaidia timu kufikia malengo,” alisema.
Mbali na Chama mchezaji mwingine ambaye mashabiki wa Singida BS wanasubiri kumuona kwa hamu kwenye michuano ya Kagame ni Khalid Aucho ambaye naye ametokea Yanga lakini kwa sasa yupo katika timu ya taifa Uganda.