:::::::
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kukatika kwa umeme kesho Jumapili, Septemba 7, 2025, kutokana na matengenezo katika kituo cha kupoza umeme cha Gongolamboto.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Septemba 6, 2025 imesema, umeme utakosekana kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 11 jioni, hatua inayolenga kuimarisha huduma kwa wateja wake wa Mkoa wa Ilala na vitongoji jirani.
Maeneo yatakayoathirika na kukatika kwa umeme ni Kisarawe, Chanika yote, Moshi Bar, baadhi ya maeneo ya Mombasa na Gongolamboto, Kivule, Kitunda, Majohe, Chuo Kikuu cha Kampala, Mbondole, Magole, Siraly Msongola, Pugu na Ulongoni. Aidha, Tanesco imesema inatambua usumbufu utakaowakumba wateja wake na kuomba radhi kwa changamoto hiyo.
Pia imewataka wananchi kuwa makini na kuepuka kugusa nyaya zilizokatika au zilizo chini kwa usalama wao, na iwapo kuna tatizo lolote wawasiliane kupitia namba 180.