DC Mpogolo azindua vitabu kwenye MwanaClick

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema utunzi wa vitabu unaofanywa na watu mbalimbali nchini ni ushahidi wa wazi wa mapinduzi chanya ambayo Tanzania imeyapitia katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Mpogolo amesema kuwa kitendo cha Watanzania kujitokeza kuandika na kuchapisha vitabu ni ishara ya jamii inayozidi kukomaa kielimu, kiutamaduni na kitaaluma, jambo linalochangia kukuza maarifa na kuongeza thamani ya fikra za kizalendo.

Mpogolo ametoa kauli hiyo leo Septemba 6, 2025 wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vilivyoandikwa na Abdulkadir Massa ambaye pia anauza vitabu hivyo kupitia programu (APP) ya MwanaClick inayosimamiwa na Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mpogolo amezindua vitabu hivyo viwili ambavyo ni “Hatima Iliyofutika na Katika Kivuli cha Ulimbukeni.

“Uandishi huu unadhihirisha hatua iliyopigwa. Ni vyema kutumia vipawa vya wengine kujifunza, tusome vitabu walivyoandika kwa sababu kusoma kunaongeza maarifa na ndiyo maana sisi wengine tunaweza kusimama na kuhutubia hata kwa saa mbili,” amesema.

Mpogolo amesema katika maisha ya kawaida watu wanatamani kuandika vitabu lakini wanashindwa kuanza.

“Kila mtu anayo historia yake anayoweza kuwasimulia watu waliopo eneo analoishi ikiwemo mahusiamo, elimu na changmoto lakini kuanza kuandika historia hiyo ni kipaji ambacho Mungu hutoa,” amesema.

Amesema upo umuhimu wa kuandika unachofikiria na kusimuliwa unahifadhi maarifa na historia kwa ajili ya vizazi vingine.

Mpogolo amesema kuna ugumu wa kuweka chini mawazo na kuyatengenezea muundo ili yaweze kusomeka, hivyo wanoandika wanasaidia kufikisha maarifa kwa watu wengine.

Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa vitabu vyake, Adbulkadir Massa ambaye ni mwandishi, amesema kuzinduliwa kwa vitabu hivyo ni kufunguliwa rasmi kwa safari ya kuelekea ndoto zake.

Ili kufanikisha hilo amesema yuko tayari kuzifuata ndoto popote zilipo, hivyo kama zimejificha nyuma ya mwamba wataupasua wazifikie, kama ziko porini watafichua na kama mapangoni watazifuata.

“Kitu cha muhimu msiache kupambania ndoto zenu na watu wa kwanza wanaoweza kuwasaidia ni watu wa karibu wanaoweza kuwafikisha mkutane na watu wengine wanaoweza kuwashika mkono,” amesema.

Amesema kuzinduliwa kwa vitabu hivyo vya Kiswahili ni kwa ajili ya kutambuliwa kitaifa kutokana na kutumia lugha ya Kiswahili na baadaye ataandika kwa ajili ya dunia ili iweze kutambua kuwa Tanzania kuna waandishi wabobevu.

“Natamani mjue kuwa hakuna jambo linalokuwa bila changamoto lakini hata zikija lazima tupambane, msikate tamaa wadogo zangu kwani hatujaumbwa kukata tamaa bali kuvuta pumzi na kuanza upya,” amesema.

Mama mzazi wa Abdulkadir, Farida Mgome amesema kama wazazi wamekuwa wakijitahidi kumuunga mkono kijana wao bila kujali ni nje ya kile anachosomea.

“Tunafanya hivi kwa sababu tangu utoto wake amekuwa mdadisi wa vitu japokuwa awali tulitaka awe daktari, yeye alichagua kuwa mfamasia na hata alipoanza kuandika vitabu tulimuunga mkono na kumpa usaidizi uliohitajika japokuwa mambo mengi aliyafanya yeye,” amesema.

Mwanzilishi wa Mkuki na Nyota, Walter Bgoya amesema kuzinduliwa kwa vitabu hivyo ndiyo mwanzo wa kazi, hususan katika kutafuta masoko huku akiwaita Watanzania kuchangamkia maarifa yanayopatikana katika usomaji wa vitabu.

Meneja Mradi wa Programu ya MwanaClick kutoka MCL, Amiri Simbano amewaalika Watanzania kusoma vitabu hivyo kwa njia ya mtandao kupitia programu ya MwanaClick inayopatikana kuputia Appstore na Google play store.

Amesema kwa watakaosoma mtandaoni watapata punguzo la bei kwani badala ya kununua kwa Sh10, 000 bei ya nakala ngumu, mtandaoni watalipia Sh3, 000 pekee kwa nakala moja.

“Nawakaribisha sana ili tuweze kumuunga mkono kijana mwenzetu ili aweze kufikia malengo yake,” amesema.