Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amerejesha fomu kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) akieleza matumaini yake ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.
Dk Mwinyi, Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anayemaliza muda wake, alikuwa wa kwanza kuchukua fomu Agosti 30 na leo Septemba 6 amezirejesha akiwa wa kwanza.
Baada ya kukabidhiwa fomu alipaswa kukamilisha masharti yaliyowekwa na ZEC, ikiwamo kupata wadhamini 200 kutoka kila mkoa kwa mikoa mitano ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu hizo, Dk Mwinyi amewashukuru wana-CCM kwa kujitokeza kwa wingi kumdhamini, jambo alilosema limemwezesha kupata idadi kubwa ya wadhamini kuliko matarajio.
Amesema amefurahishwa na utayari wa wana-CCM katika mikoa yote Unguja na Pemba waliojitokeza kwa wingi kumdhamini.
“Nawapongeza kwa dhati kwa utayari wao wa kufanya hivyo, kwani nilipata wadhamini wengi kuliko matarajio, hatimaye leo nimerudi kurejesha fomu yangu hapa nikiwa wa kwanza. Namshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kukamilisha hatua hii muhimu katika uchaguzi wetu,” amesema akieleza wanachosubiri ni uteuzi Septemba 11.
Dk Mwinyi amesema baada ya uteuzi, chama hicho kinatarajia kuzindua kampeni zake Zanzibar Septemba 13, 2025.
Akizungumzia kauli ya baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo kupitia vyama vingine wanaosema hawawezi kushindana naye na badala yake wanatafuta kuteuliwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk Mwinyi amesema wameshaona hawawezi kushindana naye.
Amesema jambo hilo halina mjadala kwani ni kweli vyama vingine haviwezi kushindana na CCM ila wao wanatakiwa kujitahidi angalau wapate asilimia zitakazowawezesha kupata nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
“Hilo halina mjadala na ndivyo ilivyo, kwamba sasa hivi wao wajitahidi kupata angalau huo umakamu na wanaosema hivyo nawashukuru kwa sababu wanaona hali halisi, ndiyo ukweli wa mambo ulivyo,” amesema.
Waliosema wanatafuta nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni mgombea wa AAFP, Said Soud Said na mgombea wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib.
Kwa nyakati tofauti wamesema wanaona kazi kubwa inayofanywa na Dk Mwinyi, lakini wao wanataka nafasi ya pili.
Hata hivyo, Dk Mwinyi amesema wanatakiwa kupambana kuipata nafasi hiyo, kwani wanaoitaka ni wengi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 chama kinachoshika nafasi ya pili kikiwa kimepata asilimia 10 ya kura zote ndicho kinapata fursa ya kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Dk Mwinyi amewataka wagombea wenzake kuweka kipaumbele cha kuhubiri amani ya nchi ili kwa pamoja waweze kudumisha amani iliyopo kwa kufanya kampeni za kistaarabu na hatimaye mshindi aweze kushika dola na kuipeleka mbele nchi kimaendeleo.
Baada ya kupokea fomu, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema hatua ya kurejesha fomu ni kwa mujibu wa kifungu cha 47 cha Sheria namba nne ya Uchaguzi Zanzibar ya mwaka 2018.

Amesema kwa sasa Tume itaipitia fomu hiyo na kujiridhisha iwapo imejazwa kwa usahihi na kama kuna changamoto muhusika atajulishwa.
Amesema baada ya kufanya uteuzi, watabandika fomu hizo katika ofisi ya Tume kwa saa 24 ili kama kuna mgombea anataka kuweka pingamizi afanye hivyo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina, amesema Tume ilitoa fomu kwa vyama 17, mmoja amesharejesha na wengine bado wanaendelea na taratibu.
Amesema ZEC inatarajia ifikapo Septemba 10 saa 10:00 jioni ndiyo mwisho kwa wote kurudisha fomu na Septemba 11 ni siku ya uteuzi.
“Tutabandika na ikiwa hakutatokea pingamizi yoyote basi wote watakwenda kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu,” amesema.