MABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji wa Namungo, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ katika kila kipindi, yameifanya timu hiyo kufuzu fainali ya mashindano ya Tanzanite Pre-Season International.
Namungo imeiondosha Tabora United kwa kichapo cha mabao 2-1, katika mchezo wa nusu fainali ya mashindano hayo uliochezwa leo Septemba 6, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Tabora United ilikuwa ya kwanza kuandika bao mapema tu dakika ya 13 kupitia Chewe Chanda.
Hata hivyo, Namungo haikuwa kinyonge, kwani licha ya kuruhusu bao la mapema, ilijipanga kwa kurudisha mashambulizi ambayo Tabora United iliyazuia ipasavyo.
Wakati mwamuzi wa mezani akionesha zimeongezwa dakika mbili baada ya kutimia 45, haikuchukua muda mrefu, Haaland akaweka mzani sawa na kufanya timu kwenda mapumziko matokeo yakiwa Tabora United 1-1 Namungo.
Kipindi cha pili, makocha wa timu zote mbili, Juma Mgunda wa Namungo na Kaunda Simonda wa Tabora United, walifanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa ili kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao.
Mabadiliko hayo yaliinufaisha Namungo kwani nguvu iliyoongezwa ilimrahisishia kazi Haaland kufunga bao la pili dakika ya 85 na kuipeleka timu hiyo fainali.
Kwa kuingia fainali, Namungo hivi sasa inamsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili itakayoanza saa 10:00 jioni ambapo Dodoma Jiji inakabiliana na City FC Abuja ya Nigeria.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yakiandaliwa na Fountain Gate FC, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni kesho Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali saa 10:00 jioni.
Jumla ya timu kumi zimeshiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A limeundwa na timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC ya Manyara.
Kundi B ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.