Babati. Waziri mstaafu Mary Nagu amewaasa wananchi wa Mkoa wa Manyara kulipa wema wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura nyingi za ndiyo katika uchaguzi ujao, akisema kuwa Rais huyo ameonyesha moyo wa huruma na kujali wananchi wake kwa vitendo.
Akizungumza leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, mjini Babati, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM Mkoa wa Manyara, Nagu amesema kuwa wananchi hawapaswi kusahau jinsi Rais Samia alivyochukua hatua ya kuahirisha ghafla ziara yake nje ya nchi baada ya kusikia kuhusu maafa makubwa yaliyotokea wilayani Hanang’.
Maafa hayo, yaliyotokea Desemba 2023 kutokana na maporomoko ya matope kutoka Mlima Hanang’, yalisababisha vifo vya watu 69, majeruhi 116, na kuathiri zaidi ya kaya 1,150.
“Rais wetu hakusubiri taarifa rasmi pekee, bali alirudi nyumbani haraka kuwa pamoja na wafiwa na waathirika wa maafa. Hii ni ishara ya uongozi wenye huruma, moyo wa kibinadamu na kujali wananchi. Tunapaswa kumlipa wema wake kwa kura za ndiyo,” amesema Nagu.
Amesisitiza kuwa moyo huo wa kujitoa kwa Rais Samia unatakiwa kuthaminiwa na kila Mtanzania, hususan wananchi wa Manyara walioguswa moja kwa moja na tukio hilo la kihistoria.
“Rais Samia kwa kweli ametuheshimisha wana Manyara kwa kutujali wakati wa maafa ya Hanang’ alifika kutufuta machozi nasi tutamshukuru kwa kumpa kura za ndiyo,” amesema Nagu.
Ameeleza kwamba japokuwa yeye aligombea ubunge mwaka 2025 kwenye kura za maoni na kura hazikutosha, watampa kura nyingi za ndiyo Asia Halamga, mgombea aliyepitishwa na CCM.
Aliyekuwa mbunge wa Babati mjini Pauline Gekul amesema Rais Samia amefanya mambo makubwa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo anastahili kupata kura nyingi za kishindo.
“Tukisema tutaje miradi iliyotekelezwa kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tutakesha kwani tumeona barabara, shule, hospitali vituo vya afya, zahanati, maji na umeme,” amesema Gekul.
Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Shaban Mrisho, amewataka viongozi, wapenzi na wakereketwa kuiga mfano wa viongozi hao waliokuwa wabunge.
“Mama Nagu na Gekul japokuwa wao hawakupitishwa na CCM kugombea ubunge lakini hawakununa,, kwani wamegudhuria uzinduzi wetu, na kutupa somo kubwa,” amesema Mrisho.
Diwani mteule wa kata ya Magara wilayani Babati, Gonzalez Mkoma ameeleza kwamba wana CCM wa Manyara wanayo kila sababu ya kutamba kwani wamejiandaa vilivyo kumpa kura za ushindi Rais Samia.
“Manyara kura za kutosha zinamsubiri mama Samia na tunaposema Oktoba tunatiki tuna maanisha hivyo hatuna jambo dogo,” amesema Mkoma.
Mdau wa maendeleo wa mkoa huo, Taiko Kulunju amesema wana Manyara watampa kura nyingi za ndiyo mgombea urais wa CCM Samia kutokana na miradi mingi ya maendeleo aliyoifanya.
“Mama Samia amemwaga fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, maji na miundombinu ya nishati ya umeme, wana Manyara tuna deni naye tutamlipa kura za kutosha,” amesema Taiko.