Hekaya za Mlevi: Zishtukieni sera za ndoto 

Dar es Salaam. Mimi sijui nina uraibu gani. Hata akipita mwendawazimu anayeongea peke yake, nitahangaika hadi nisikie kile anachosema. Mara kadhaa nimekuwa nikiwasikiliza paka wanaolalama usiku wa manane, nikawa nasikia kama wanaongea kama watu. Wakati mwingine niliogopa kwa kudhani nagombaniwa miye, maana mmoja alisema “ni wanguuu” mwingine akajibu “mwongooo”. 

Kwa kutaka kujua kila kitu, najikuta nikifungulia redio, TV na huku nikiwa nimekumbatia gazeti. Kisa ni kutaka kujua kila kinachoendelea duniani. Kila siku huwa nasoma gazeti zima hadi barua za wasomaji kwa hofu ya kupitwa. Kwa bahati nzuri baada ya saa sita za usiku redio na TV hupiga muziki tu, hapo ndipo napata kula na kulala. 

Vinginevyo kila siku ningekuwa nakesha na njaa, maana hata njaa hukosa nafasi mbele ya habari za motomoto. Hali hii imeongezeka wakati huu wa hekaheka za uchaguzi. 

Nimekuwa nikimsikiliza kwa makini kila mgombea anayefanya kampeni. Na nilivyo na uwezo wa ajabu, naweza kushika kadiri ya robo tatu ya yote ninayotazama, kuyasikiliza na kuyasoma kwa wakati mmoja. Wakati mwingine hujikuta nimepitiwa na usingizi, na ikifikia hatua hiyo huwa najilaumu sana kwani siwezi kuzirudisha nyuma hotuba zao.

Leo nimejifungia chumbani tangu asubuhi nikisikiliza kila kipande. Hapa kuna mgombea atakayegawa utajiri kwa wananchi hata watakaolala maisha yao yote, huku kuna atakayegawa bodaboda za bure kwa kila kijana wa Kitanzania… ama kweli kampeni zina mambo. Kuna atakayejenga viwanja vya ndege kwenye kila kijiji hata kama kina watu watano. Japo nilihisi uchovu lakini sikuacha kufuatilia.

Kwa mbali nikaanza kuhisi kama vile nami nipo katika mkutano wa kampeni. Cha ajabu maeneo yalibadilika kila baada ya muda mfupi. Mwanzo tulikuwa jangwani ambapo wakazi tulikuwa na shida ya chakula na maji. 

Akatujia mgombea mmoja mnene sana, mwenye nguo chakavu. Akatuambia hatatuletea maji, bali ataligeuza jangwa lile kuwa kituo cha utalii. Kila mtu aliguna; je akitutimua na kukigawa kijiji chetu kwa mwekezaji?

Mara tukajikuta tupo katika moja ya maghorofa yaliyotapakaa nchi nzima. Mgombea akatuambia tukimchagua atatukabidhi kila mmoja ghorofa lake. Tukamwuliza tutapata wapi chakula na fedha? Yeye akajibu “hamjui kuwa ghorofa ni utajiri?”

Hatukuelewa kwa sababu hakuna wa kumuuzia maana hakukuwa na mwenye fedha, na huwezi kupangisha kwa kuwa kila mtu angekuwa na ghorofa lake. 

Kisha akatokea mgombea aliyekuwa mrefu na mwembamba sana. Alivalia nguo za hariri zilizong’ara kama jua. akatupeleka angani kwenye nyota na sayari. Akatuambia tukimchagua atatuhamishia kwenye sayari zingine maana dunia imeshachakaa. Mmoja wetu akauliza kwa nini tusiboreshe mazingira na kuishi kama peponi, akamjibu “huu si wakati wa kulima na kuchimbua udongo. Ni wakati wa sayansi, teknolojia na akili mnemba!”

Nilishtuka kutoka usingizini. Kumbe nilikuwa naota. Lakini nilipoifikiria ndoto yangu niligundua kuwa haina tofauti sana na mambo yanayoendelea wakati huu. Mara zote wagombea wetu wananadi maendeleo na mafanikio, wanaacha kutuambia jinsi watakavyoshughulika na matatizo yetu. Maendeleo yanawezaje kuwepo bila kuondoa changamoto zilizopo? Au labda ndio sera ya kuihama dunia na kwenda kuishi kwenye sayari mpya.

Tumeyasikia mengi yakiwemo ya elimu bure, matibabu bure, makazi na usafiri bure. Hizi sekta zitakazotoa huduma ya bure zitapewa au kuokota vitendea kazi? Ajira hakuna na mnawataka watu wajiajiri. Sasa walimu na wauguzi waliojiajiri watatoa huduma bure? Serikali ikitoa huduma hizo bure, watu hawatakuwa na sababu ya kuhudumiwa na sekta binafsi kwa kukwepa gharama. Basi nini maana ya kujiajiri? 

Kadri kampeni zilivyoendelea, sera zinageuka kuwa mashindano ya mzaha. Kila mgombea anataka kumzidi mwenzake. Wa kwanza akiahidi kupanda miti ili kupata mvua za kutosha, wa pili atanadi kutengeneza mvua kwa akili mnemba. Akitokea wa tatu, basi atagawa app ya kupakua mvua kwa kutumia simu janja! Wa nne atagawa bando la bure ili kila mmoja ajipakulie mahitaji yake. 

Uzuri wa binadamu, anaporidhishwa anaridhika. Mtu mwenye shida huwa na hasira, lakini akipewa ahadi tamutamu anaweza kusahau shida zake na kuziishi ahadi alizopewa. Watoaji wa ahadi nao kwa kulitambua hilo hawafanyi makosa wanajua wapi akipuliza moto utawaka na wapi utazima. Mchungaji mmoja aliwatisha watu walioishi kwenye baridi kali kwamba wakitenda dhambi, watatupwa kwenye jehanamu ya barafu! 

Vivyo hivyo watakuja wagombea viti na sera za aina hiyo. Mmoja atasimama katikati ya Dar es Salaam na kusema “mkinichagua nitaondoa joto kwa kufunga mashine kubwa ya kupoza hewa angani”. Maneno hayo akienda nayo Mufindi atafeli, lakini atayatumia hayohayo baada ya kuyahariri kidogo ataligeuza neno “joto” kuwa “baridi” na “kupoza” liwe “kupasha”. Huku alisema “Dar safi”, kule atasema “Mufindi safi”.

Nataka niifananishe hii na jamaa mmoja aliyeitwa “Kidume”. Shughuli yake ya kutwa nzima ilikuwa ni kubadilisha wasichana. Katika barua zote alizowaandikia alitumia maneno yaleyale, kilichobadilika ni jina la mpokeaji tu. Sasa nawashtua wapigakura na wananchi kwa ujumla jihadharini na watoa ahadi wanaokopi na kupesti. Kila eneo lina shida zake. Kama kweli wanazijua shida zenu, wahangaike nazo kivyenu.