JamiiForums yafungiwa, mmiliki ajiuzulu ujumbe wa bodi

Dodoma. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imelifungia jukwaa la mtandaoni JamiiForums kwa miezi mitatu, huku mmiliki wa mtandao huo Maxence Melo akijiuzulu ujumbe wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

TCRA kupitia taarifa iliyotolewa leo Septemba 6, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk Jabir Bakari imesema leseni iliyotolewa kwa Vapper Tech JamiiForums imesitishwa kwa kipindi hicho kuanzia leo Septemba 6.

“JamiiForums kupitia jukwaa lake na akaunti zake za mitandao ya kijamii ilichapisha maudhui ya kupotosha umma, kukashifu na kudhalilisha Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na Marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025,” imeeleza taarifa ya TCRA na kuongeza:

“Pamoja na kukiuka kanuni, maudhui hayo yanakinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania, jambo ambalo linaathiri umoja, amani na mshikamano wa kitaifa na kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

TCRA imefafanua kupitia taarifa hiyo kuwa kwa mamlaka iliyopewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura 306, imesitisha kwa muda wa siku 90 kuanzia Septemba 6, 2025 leseni ya Huduma za Maudhui Mtandaoni iliyotolewa kwa Kampuni ya Vapper Tech Limited (JamiiForums) na kuzuia upatikanaji wa jukwaa la JamiiForums.

Kwa upande wake, mmiliki wa mtandao huo Melo, kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram amesema amemuandikia Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu uamuzi wa kujiuzulu ujumbe wa Bodi katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuanzia leo Septemba 6, 2025.

“Niliteuliwa Desemba 18, 2023 na nimehudumu kikamilifu majukumu yangu. Natoa shukrani nyingi kwa Wizara, Tume na wajumbe wenzangu kwa ushirikiano mzuri walionipa katika kipindi chote,” ameandika na kuongeza:

“Aidha, naishukuru taasisi yangu na Bodi ya Wakurugenzi kwa kulipa gharama zote za ushiriki wangu katika vikao vyote na shughuli za Tume kwa takribani miaka miwili.”

Awali, jana Septemba 5, Melo alieleza kuwa kuna uvamizi usio rafiki umefanyika katika ofisi zao zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, akidai wavamizi walikuwa wakimtafuta yeye.

Baadaye Serikali ilisema haukuwa uvamizi bali ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano na kumtaka kutoa ushirikiano na asizue taharuki katika jamii.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram Septemba 5, 2025 Melo aliandika: “Kuna uvamizi usio rafiki uliofanyika muda siyo mrefu katika ofisi za JamiiForums, Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakinitafuta mimi. Nalaani vitendo kama hivi, ila umma utaujua ukweli hivi karibuni.”

Hata hivyo, hakufafanua ni kina nani waliohusika na uvamizi huo, wala sababu zilizowafanya kuingia katika ofisi hizo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake wa X aliandika akisema hakuna uvamizi uliofanyika katika ofisi za Jamii Forums.

“Kilichotokea ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano kati ya mamlaka za Serikali na wadau wake ambapo leo maofisa wa Serikali walikwenda kuwasilisha barua ya wito kwa Jamii Forums. Ndugu Maxence Melo usilete taharuki isiyo na sababu za msingi, toa ushirikiano.”

JamiiForums ni moja ya majukwaa makubwa ya mtandaoni nchini Tanzania yanayojulikana kwa mijadala ya masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.