JamiiForums Yafungiwa Siku 90 na TCRA kwa Maudhui Yenye Utata – Global Publishers



Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda wa siku 90 leseni ya huduma za maudhui mtandaoni ya kampuni ya Vapper Tech Limited, wamiliki wa jukwaa maarufu la JamiiForums, kufuatia tuhuma za kuchapisha maudhui yanayodaiwa kupotosha na kudhalilisha viongozi wa Serikali.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Septemba 6, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, mamlaka hiyo imesema mnamo Septemba 4, JamiiForums ilichapisha taarifa mtandaoni kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 pamoja na marekebisho ya mwaka 2022 na 2025, kwa madai ya kushusha heshima ya Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

TCRA imeeleza kuwa maudhui hayo si tu kwamba yamevunja kanuni, bali pia yamekiuka mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania kwa kuhatarisha mshikamano wa kitaifa na amani ya kijamii.

“Kutokana na mamlaka tuliyopewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, TCRA imesitisha kwa muda wa siku tisini (90) kuanzia leo Leseni ya Huduma za Maudhui Mtandaoni iliyotolewa kwa Vapper Tech Limited (JamiiForums),” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa hatua hii, upatikanaji wa JamiiForums umesitishwa kwa kipindi cha siku 90, huku TCRA ikisisitiza umuhimu wa wamiliki wake kuzingatia masharti ya leseni na kanuni husika kabla ya kurejea hewani.