ALIYEKUWA Kocha wa Bigman, Zubery Katwila amejiunga na Geita Gold kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya dili lake la kwenda Coastal Union ya Tanga iliyofanya mazungumzo naye mwanzoni ya kumhitaji kuingia dosari.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zimelidokeza Mwanaspoti kuwa Katwila amesaini mkataba wa mwaka mmoja na muda wowote kuanzia sasa atajiunga kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi ya Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na dili hilo, Katwila alisema hakuna makubaliano yaliyofikiwa kwa sababu kwa sasa amepumzika, ingawa kama kutakuwa na taarifa zozote za sehemu atakayokwenda msimu ujao mashabiki wa soka watajua.
“Nikipata timu ya kwenda basi utajua na hata mashabiki zangu watajua pia. Mkataba wangu na Bigman ulikuwa wa mwaka mmoja tu ambao umeisha msimu uliopita, nikiongeza au kama nitaenda kutafuta changamoto sehemu mpya mtaona,” alisema Katwila.
Kocha huyo aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar, alijiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’ aliyejiunga na Pamba ambayo kwa sasa ameachana nayo.
Katika msimu wa 2024-2025, Katwila aliiwezesha Bigman kumaliza nafasi ya nane katika Ligi ya Championship na pointi 47 baada ya kushinda mechi 12, sare 11 na kupoteza saba ikifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024 katika msimu wa 2024-2025 wa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56 chini ya Kocha Mkuu Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara baada ya kupoteza mechi za mchujo.
Timu hiyo ilicheza mchujo ili kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya sare nyumbani ya mabao 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2