Kipa Mzenji awataja Camara, Diarra

KIPA wa zamani wa Azam FC, Ahmed Salula anayeichezea Uhamiaji ya Zanzibar amesema makipa Djigui Diarra wa Yanga na Moussa Camara wa Simba ni chachu ya ushindani katika nafasi hiyo kwa wengine kutokana na viwango walivyo navyo vilivyowafanya kuaminiwa vikosini.

Salula ambaye ni askari wa Jeshi la Uhamiaji, amesema anawafuatilia makipa hao wawili wa kigeni na amekuwa anajifunza jinsi ya kujiamini, umakini na utulivu katika kuokoa mipira ya hatari, hivyo sio dhambi wazawa kuiga vitu kutoka kwao.

“Kazi ya mpira ni kujifunza kila wakati. Camara na Diarra wamefanya kazi nzuri inayovutia. Sina maana wazawa hawafai, wapo wengi tu wanaocheza vizuri kama Yakoub Seleiman aliyetoka JKT Tanzania kwenda Simba, Aishi Manula japo kwa hivi karibuni sijamwona akipata nafasi ya kudaka, Yona Amos wa Pamba. Hao ni baadhi wenye uwezo mkubwa langoni,” alisema.

Selula aliyewahi kuzichezea KMKM na Malindi, pia alizungumzia ujio wa Kocha Florent Ibengé Azam FC, anapaswa kupewa ushirikiano ili kuhakikisha wanafikia malengo.

“Ni kocha mwenye CV kubwa, lakini timu nzima inatakiwa kuwa kitu kimoja kuhakikisha wanatimiza malengo ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ambao walichukua mara moja mwaka 2014.

Hivyo kocha, wachezaji na viongozi kila mmoja atimize wajibu wake,” alisema Salula aliyeiwezesha Uhamiaji msimu uliopita kumaliza Ligi Kuu Zanzibar katika nafasi ya sita.