KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema ongezeko la kiungo mshambuliaji Sospeter Bajana litainufaisha timu hiyo kutokana na kipaji na uwezo alionao.
Ahmad alisema anaufahamu uwezo wa Bajana kwani aliwahi kufanya naye kazi walipokuwa KMC na ni miongoni mwa vipaji vikubwa nchini, hivyo anatarajia ataongeza ushindani wa namba kikosini.
Bajana amejiunga na JKT Tanzania akitokea Azam FC iliyomuaga hivi karibuni na Kocha Florent Ibenge alimwambia timu hiyo ni kama nyumbani kwake wakati wowote anaojisikia anaweza kurejea.
Ahmad alisema: “Bajana ni mpambanaji kuanzia mazoezini ambako anajituma kwa bidii hadi mechi za mashindano anazokuwa anajitolea kuhakikisha timu inapata ushindi.
“Ana nidhamu ya hali ya juu katika kazi yake. Siyo mchezaji wa kumfuatilia katika ratiba za timu, anajitambua na kujua anatakiwa kufanya kitu gani na kwa wakati gani.”
Bajana aliwahi kuwa kiungo tegemeo Azam FC hadi akakabidhiwa unahodha wa kikosi hicho enzi za kocha Youssouph Dabo, lakini majeraha aliyoyapata yalimtibulia kwani alitumia muda mrefu akiwa nje ya uwanja.
Mbali na hilo, kocha huyo alisema wanaendelea na maandalizi ya msimu mpya unaotarajia kuanza Septemba 17 na siku moja kabla itachezwa mechi ya ufunguzi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga.
“Tunaendelea na maandalizi hadi tutakapoanza majukumu ya ligi kwa asilimia kubwa. Kimbinu vitu vingi vimekamilika,” alisema.