Mafuwe aahidi soko la kisasa kwa wafugaji wa Kia

Hai. Mgombea ubunge wa Jimbo la Hai kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Saashisha Mafuwe, ameahidi kutumia ushawishi na mahusiano yake ndani ya Serikali kuhakikisha soko la mnada wa mifugo lililopo katika eneo la Mijohoroni, Kata ya Kia, linaboreshwa na kujengwa kwa viwango vya kisasa.

Amesema lengo la maboresho hayo ni kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao katika mazingira bora, salama na yenye tija zaidi kwao na jamii kwa ujumla.

Mafuwe alitoa ahadi hiyo jana, Septemba 5, 2025, wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kia katika mkutano wa hadhara wa utambulisho wa madiwani wa kata 17 za Jimbo hilo.

Alisema ujenzi wa soko hilo ni moja ya vipaumbele vyake ikiwa atapata ridhaa ya wananchi kurejea bungeni, kwa kuwa linahusiana moja kwa moja na kuinua kipato cha jamii ya wafugaji wilayani humo.

“Najua hapa mlipo soko hili bado halijafanana na wilaya hii, lazima tutengeneze mazingira ya soko hili likae kwa mfumo wa kuwa soko linalofanana na Wilaya ya Hai.

“Tutalifanya hili soko kuwa la kisasa, lenye miundombinu ya kudumu, ili wafugaji wasiende mbali kuuza mifugo yao, hili ni jambo linalowezekana, na nitahakikisha tunalifanikisha kwa kushirikiana na Serikali kuu,” alisema.

Pamoja na soko hilo, alisema tayari Serikali ina mpango wa kujenga machinjio ya kisasa ndani ya kata hiyo.

“Ninyi ni mashahidi tumejenga majosho kule, visima vya umwagiliaji pamoja na mambo mengine, lengo ni kuhakikisha mnafanya shughuli zenu katika mazingira rafiki na yenye tija,” alisema Mafuwe.

Akizungumza katika mkutano huo, Felista Njau, ambaye alikuwa mtiania wa ubunge Jimbo Moshi Vijijini, alisema wananchi wa jimbo la Hai wanacho cha kujivunia kwa kuwa walimpata kiongozi muwajibikaji na kuwataka wasifanye makosa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Wananchi wa Hai mna kijana mpambanaji, mshikilieni hakikisheni Oktoba 29 mnampigia kura za kutosha ili aendelee kuwapambania kuwaletea maendeleo zaidi,” alisema Njau.

Akizungumzia changamoto ya soko hilo, Baraka Lazier alisema soko hilo halina miundombinu ya kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira rafiki.

“Tunamwomba Saashisha kama ataendelea kipindi cha pili ahakikishe soko hili linajengewa miundombinu, maana hakuna huduma yoyote na jua ni kali,” alisema mwananchi huyo.