Makada 18 wa Chadema washikiliwa na polisi

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikiliwa watuhumiwa 18, akiwamo Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Felius Kinimi, wakituhumiwa kufanya mikusanyiko iliyo kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao leo Septemba 6, 2025, akisema wamekamatwa eneo la Sambarai Kibosho, wilayani Moshi.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikiliwa watuhumiwa 18, akiwamo Katibu Mwenezi wa Baraza la Vijana Taifa, Chadema kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko iliyo kinyume cha sheria sambamba na kupanga njama za kuhamasisha vurugu na kuhatarisha amani na usalama nchini,” imeeleza taarifa ya Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, limekuwa likiwafuatilia sambamba na kukusanya ushahidi na leo Septemba 6, walipokuwa wanakwenda kutekeleza vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria ndipo likawatia nguvuni.

“Ushahidi unakamilishwa ikiwa ni sambamba na kuwahoji ili hatua nyingine za kisheria zifuate,” imeeleza taarifa hiyo.

Jeshi hilo limetoa onyo kwa yeyote anayepanga njama za kuhamasisha na kufanya vurugu ili kuhatarisha amani, utulivu na usalama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu na baada ya uchaguzi halitasita kuwakamata ili sheria ichukue mkondo wake.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel imesema msafara wa viongozi wa Bavicha Taifa na kanda hiyo ukiwa njiani kuelekea nyumbani kwa kina Deusdedith Soka kama sehemu ya kuenzi mashujaa wa chama hicho polisi walizuia msafara wao.

Soka alitoweka takribani mwaka mmoja umepita na hajawahi kuonekana.

“Magari ya polisi yamezuia msafara huo takribani mita 100 kutoka barabara ya Kibosho, mkoani Kilimanjaro. Ni dhahiri kuwa hatua hii haikuwa ukaguzi wa kawaida, bali ni dhamira mahususi ya kuzuia msafara kuendelea na shughuli zake kwa amani,” imeeleza taarifa ya Chadema na kuongeza:

“Idadi ya magari ya polisi imekuwa ikiendelea kuongezeka eneo la tukio, jambo linalozua hofu na kuashiria nia ya kuchochea vurugu na kuvunja amani badala ya kuilinda. Tunalisihi Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kuacha mara moja vitendo vya uchochezi na matumizi mabaya ya nguvu, wajibu wa msingi wa polisi ni kulinda usalama na amani ya raia wote bila upendeleo.”

Welwel katika taarifa hiyo amesema: “Chadema hatutatishwa wala kukatishwa tamaa na mbinu ovu za kuzuia harakati halali za kidemokrasia. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu hatua zote zinazochukuliwa na tutasimama imara katika kulinda haki, amani na demokrasia nchini mwetu.”