Lindi. Mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa, muda mfupi baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wake wa kampeni.
Tukio hilo limetokea leo, Jumamosi Septemba 6, 2025, katika uwanja wa Shule ya Msingi Mpilipili, ambapo Mchinjita ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara) alikuwa akizindua rasmi kampeni zake za kuwania ubunge kwa mara nyingine, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo uwanjani hapo, polisi walimchukua Mchinjita mara tu baada ya kushuka jukwaani, na mpaka sasa haijafahamika sababu rasmi za kushikiliwa kwake.
Hata hivyo, Mwananchi Digital limezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori aliyesema hana taarifa za kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho, akiahidi apewe muda wa kufuatilia.
“Nipo Ruangwa sijapata bado taarifa za kukamatwa kwa viongozi wa ACT-Wazalendo, ngoja nifuatilie nitakujuza,” amesema Kamanda Imori.
Akisimulia tukio hilo, lilivyokuwa Katibu wa ACT-Wazalendo Jimbo la Lindi Mjini, Ahmad Zuber amesema walikuwa wanamsindikiza Mchinjita akiwa ameambatana na viongozi wenzake.
“Wametupiga mabomu wakati tunatoka kwenye mkutano wa kampeni, huku wakiwachukuwa viongozi wetu na vijana wawili ambao bado hawajatambulika. Bado tuna hofu kutokana na tukio hili,” amesema Zuber.
Naibu Katibu wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo amesema, “ni kweli wamekamatwa, tumepata hizo taarifa na sisi tunafuatilia kwa ukaribu kujua kilichojiri hadi kiongozi wetu kukamatwa,” amesema Ayo.