Dar es Salaam. Waokota taka rejea jijini Dar es Salaam wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kazi yao ya kukusanya na kuuza taka zinazoweza kutumika tena, wakitaja kunyanyapaliwa na jamii, bei duni, mizani ya udanganyifu na kutotambuliwa rasmi na Serikali kuwa miongoni mwa matatizo yanayowakwamisha.
Kupitia mkutano uliofanyika leo, Septemba 6, 2025, katika eneo la Masenze, wanachama wa Mtandao wa Waokota Taka Rejea Dar es Salaam (Mtawada), wamekutana kujadili namna ya kutafuta suluhu ya changamoto hizo zinazowakabili kila siku.
Makamu Mwenyekiti wa Mtawada Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mohamed, amesema licha ya kutembea umbali mrefu kwa siku kukusanya taka, bado wanakumbwa na bei duni kutoka kwa wanunuzi, hali inayowakatisha tamaa.
“Mtu unaweza kutembea kilomita 15 hadi 45 kwa siku, ukakusanya kilo 10 hadi 15 kwa wazee, vijana wanakusanya hadi kilo 25. Lakini unakuta bei inashuka hadi Sh350 kwa kilo, ikiwa juu sana ni Sh500. Kuna wakati bei hushuka hadi Sh100 tu kwa kilo,” amesema Mohamed.
Ameongeza kuwa kinachoumiza zaidi ni kuona kuwa wazalishaji wa taka kama chupa hupata hadi Sh500 au Sh1,000 kwa chupa moja, huku wao wanaofanya kazi ya kuzitafuta na kuzikusanya wakilipwa ujira mdogo.
“Ni vyema viwanda vikaweka mfumo wa kutoa motisha kwa waokota taka, hata kama ni ujira mdogo, kama sehemu ya kutambua mchango wetu katika usafi wa mazingira,” amependekeza.
Kwa upande wake, mjumbe wa Mtawada kutoka Kawe, Lilian Mahenge, amesema wanakutana na unyonyaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya wanunuzi ambao hubadilisha vipimo vya mizani ili kupunguza uzito halisi wa mizigo yao.
“Mzigo ukiupima sehemu tatu tofauti, utapata matokeo tofauti. Kwa mfano mzani mmoja utapata kilo 9.9, mwingine kilo 9.0. Ile pointi 0.9 imeenda wapi,” amesema Lilian.
Amesema pia kuna baadhi ya mawakala hukata kilo mbili kutoka kwenye mzigo, wakidai kuwa ni fidia ya taka zisizokubalika, hata pale ambapo mzigo huo ulikaguliwa kabla ya kupimwa.
Muokota taka mwingine kutoka Kunduchi, Yakobo Lukasi, amesema wanakumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo mazingira magumu ya kazi na kukosekana kwa utambuzi rasmi kutoka serikalini.
“Sisi ni kama makundi mengine ya wafanyakazi, lakini Serikali bado haijatupa utambulisho rasmi. Hatuna vitambulisho, mafunzo wala ruzuku. Hii inatufanya tuendelee kuonekana kama watu wasio na mchango,” amesema Lukasi.
Waokota taka hao wameiomba Serikali kuwaona kama wadau muhimu wa mazingira na kuwapatia mazingira rafiki ya kufanyia kazi, ikiwemo utambulisho rasmi, mafunzo ya usalama kazini na vifaa kinga.
Akizungumzia kwenye mkutano huo, Ofisa Afya na Mazingira wa Wilaya ya Kinondoni, Nancy Zakayo, amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mtawada katika kuhifadhi mazingira, na iko tayari kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili.
“Tunatambua mchango wao, ndio maana hata sasa ukitembea huoni tena chupa nyingi mitaani. Tupo tayari kushirikiana nao moja kwa moja kukabiliana na changamoto zozote,” amesema Nancy.
Ameongeza kuwa Wilaya ya Kinondoni imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano kuhakikisha wananchi wanatenganisha taka majumbani kwa ajili ya kurahisisha kazi ya waokota taka.
Aidha, waokota taka wametakiwa kujenga mahusiano ya karibu ili kuondoa unyanyapaa, huku wakiombwa kujiunga rasmi na Mtawada kwa ajili ya kupata misaada na ulinzi wa kijamii.