KOCHA wa timu ya Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema kikosi hicho kina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2026, dhidi ya Niger itakayopigwa Septemba 9, kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.
Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya timu hiyo kushindwa kuwika juzi ugenini kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, mbele ya Congo Brazzaville, hivyo kikosi cha Morocco kukata tiketi rasmi ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2026.
Akizungumzia sare ya timu hiyo, Morocco alisema baada ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi ya ndani (CHAN) kumalizika, nyota wa kikosi hicho walirudi nyumbani ili kupumzika, hivyo hawakuwa fiti kwa kiwango kilichotakiwa.
“Baada ya hapa na Congo fitinesi ya wachezaji itarudi katika hali yake ya kawaida na tunaamini mechi yetu ijayo dhidi ya Niger tutafanya pia vizuri,” alisema Morocco aliyeipeleka timu hiyo hadi hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024.
Katika mechi hiyo iliyoisha sare ya 1-1, bao la Stars lilifungwa na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, dakika ya 84, akitumia dakika tisa tu uwanjani tangu aingie dakika ya 75, akichukua nafasi ya Mudathir Yahya.
Bao hilo la Stars lilitokana na pasi nzuri iliyopigwa na mshambuliaji, Clement Mzize na kumkuta Gomez aliyetumia ufundi wa kusawazisha, baada ya kikosi hicho kutanguliwa na wenyeji dakika ya 68, kupitia kwa nyota wa Congo, Dechan Moussavou.
Sare hiyo ya Stars imeifanya timu ya taifa ya Morocco ‘The Atlas Lions’, ambao ni mabingwa wa CHAN 2024 kwa wachezaji wa ndani kufuzu rasmi Kombe la Dunia mwaka 2026, baada ya juzi pia kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0, dhidi ya Niger.
Morocco imefuzu hatua hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 18 katika kundi la E ikishinda mechi zote sita ilizocheza hadi sasa, ikifuatiwa na kikosi hicho cha Taifa Stars kinachoshika nafasi ya pili kufuatia kukusanya pointi zake 10.
Katika kundi hilo la E, Zambia inashika nafasi ya tatu na pointi sita ambazo ni sawa na za Niger inayoshika nafasi ya nne, ikifuatiwa na Congo iliyo ya tano na pointi moja tu baada ya sare na Stars, huku Eritrea ikijiondoa mashindanoni.
Stars inakutana na Niger huku ikiwa na kumbukumbu nzuri mechi ya mwisho zilipokutana kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, kwani kikosi hicho kilishinda bao 1-0, Novemba 18, 2023, lililofungwa na kiungo nyota wa timu hiyo, Charles M’Mombwa.