Morocco yafuzu Kombe la Dunia, Stars yabakiza mbili

Morocco imekuwa timu ya kwanza ya Taifa barani Afrika kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 nyumbani dhidi ya Niger jana, Septemba 5, 2025 huku Taifa Stars ikibakiza mechi mbili.

Ushindi huo ambao Morocco imeupata katika Uwanja wa Prince Moulay Abdallah jijini Rabat, umeifanya ifikishe pointi 18 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika kundi E jambo ambalo limeifanya ijihakikishie siti yake katika fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Mabao matano ambayo Morocco iliyapata jana, yamewekwa kimiani na Ismael Saibari aliyepachika mawili pamoja na Hamza Igamane, Ayoub El Kaabi na Azzadine Ounahi ambao kila mmoja alifumania nyavu mara moja.

Katika mchezo huo, Niger walilazimika kucheza pungufu kwa dakika 64 kutokana na mchezaji wao Abdoul-Latif Goumey kuonyeshwa kadi nyekundu mapema katika dakika ya 26 na Refa Ndala Ngambo kutoka DR Congo.

Morocco ina kumbukumbu nzuri na fainali za Kombe la Dunia kwani zilipofanyika mwaka 2022, timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya nne huku ikiweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Mechi nyingine ya Kundi E jana ilikuwa ni baina ya Congo na Tanzania iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo bao la wenyeji lilipachikwa na Dejan Moussavou huku lile la Tanzania likifungwa na Selemani Mwalimu.

Tanzania sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E ikiwa na pointi 10 na imeendelea kuwa na matumaini ya kufuzu kupitia mechi za mchujo iwapo itamaliza hatua ya makundi ikiwa miongoni mwa timu nne zilizomaliza na idadi kubwa ya pointi katika nafasi ya pili.

Tanzania imebakiza mechi dhidi ya Zambia na Niger ambazo ikishinda itakuwa na pointi 16.

Misri nayo imejiweka karibu na kufuzu Kombe la Dunias 2026 baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Ethiopia.

Mabao yaliyofungwa na Mohamed Salah na Omar Marmoush kwa mikwaju ya penalti yalitosha kuifanya Misri ifikishe pointi 19 na kuongoza msimamo wa kundi A.

Misri sasa inahitaji ushindi wa aina yoyote katika mchezo unaofuata ambaon itakabiliana na Burkina Faso ugenini, Jumanne ijayo ili ijihakikishie rasmi kwenda Kombe la Dunia.

Uganda imefufua matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Nelson Mandela baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji.

Kwa kupata ushindi huo, Uganda imesogea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa G ikifikisha pointi 12 huku kinara Algeria ikiwa na pointi 18.

Walioifungia Uganda jana ni Rogers Mato aliyeweka kimiani mabao mawili na mengine yalifungwa na Allan Okello na Elio Capradossi.

Sudan Kusini 1-4 DR Congo

Djibouti 0-6 Burkina Faso

Lesotho 0-3 Afrika Kusini