Mtandao mpya wa kuwatafutia wabunifu mitaji wazinduliwa

Dar es Salaam. Wamiliki wa kampuni changa za kibunifu (Startups) huenda wakawa mbioni kuondokana na changamoto ya mitaji baada ya kuzinduliwa mtandao utakaowaunganisha na wawekezaji.

Uzinduzi wa mtandao huo umefanyika wakati ambao mtaji ni kilio kwa wabunifu, hali inayosababisha mawazo yao kushindwa kuendelea na kuleta tija iliyokusudiwa kwa jamii.

Mtandao ujulikanao Malaika (Rhapta Angels Investor Network) unalenga kutimiza ndoto za waanzilishi wa startups wanaotaka kukuza miradi yao ya ubunifu.

Mshirika na Meneja wa mtandao huo, Musa Kamata amesema utawaleta pamoja wawekezaji na kuwasaidia kutambua fursa zilizopo.

“Lengo ni kuwaleta pamoja watu wenye nia ya kuwekeza katika startups. Uwekezaji si lazima uwe wa kifedha pekee bali unaweza kuwa katika mfumo wa ulezi wa kitaalamu na kuwaunganisha wabunifu na wawekezaji wengine,” amesema.

Kamata amesema wapo wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi, lakini hawana taarifa juu ya fursa zilizopo jambo ambalo litafanyiwa kazi na mtandao huo.

“Kuna pengo kubwa pia la ufadhili wa startup nchini kwa sababu taasisi za kifedha huwa na wasiwasi kuhusu bunifu changa kutokana na ukweli kwamba, mara nyingi hutumia mifumo ambayo haijathibitishwa,” amesema.

Kwa mujibu wa African Business Angel Network (ABAN), Dola za milioni 22.5 za Marekani (Sh56.385 bilioni) zimekusanywa kwa ajili ya miradi ya ubunifu 408 ya hatua za mwanzo hadi kufikia mwaka 2025. Mtandao huo unalenga kukusanya Dola milioni 80 (Sh200.48 bilioni) ifikapo mwaka 2027.

Meneja wa Programu ya UNDP Funguo, Joseph Manirakiza amesema kuna miradi mingi ya kijamii yenye uwezo wa kukua lakini haipati fedha kutoka benki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema amekuwa mwekezaji Malaika kwa miaka minne iliyopita, akimiliki hisa katika mawazo manane ya kibunifu lakini ni moja pekee linalotoa faida.

“Kuna msisimko mkubwa katika kila hatua kwa sababu hata pale ambapo hakuna faida, tunajifunza mambo mapya njiani. Unapata kufahamu fursa na uwezekano mpya,” amesema.