Dar es Salaam. Mamlaka za Serikali zimeutaka umma kusaidia kuwezesha kupatikana mwanamke ambaye kupitia mitandao ya kijamii ameonekana akimnywesha mtoto mdogo kunywa pombe, tendo ambalo ni kinyume cha sheria.
Jeshi la Polisi katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Septemba 6, 2025 limeeleza limeona picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii akionekana mwanamke akimhamasisha na kumnywesha pombe mtoto mdogo jambo ambalo ni ukatili kwa mtoto na ni kinyume cha sheria za nchi.
Sheria hizo zimetakwa kuwa ni Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na Urekebu wa mwaka 2023 kifungu cha 9 (3) na 13 pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na Urekebu wa mwaka 2023 kifungu cha 169 A.
“Ufuatiliaji wa kina umeshaanza kama tukio hili limetokea ndani ya nchi yetu ili kuweza kumpata huyu aliyekuwa anafanya kitendo hicho kama inavyoonekana kwenye picha mjongeo hiyo,” imesema taarifa ya jeshi hilo.
Jeshi hilo limetoa wito kwa yeyote anayemfahamu mwanamke huyo asisite kutoa taarifa kwa njia yoyote atakayoona inafaa na ni rahisi kwake au kupitia namba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi 0699 998899.
“Aidha, tunamtaka mwanamke huyu akiona taarifa hii ajisalimishe mwenyewe katika kituo chochote cha polisi,” imeeleza taarifa hiyo kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ameadika: “Wengi sana mnanitumia video ya madai ya huyu binti/msichana/mama hapo kwenye picha kuwa anampa mtoto kinywaji cha pombe. Ikiwa madai haya ni ya kweli, hili ni kosa kisheria. Ili kuthibitisha madai haya, uchunguzi wa Polisi unahitajika @polisi.tanzania 0699 998899 hivyo, tunahitaji wote kutoa taarifa Polisi ili zisaidie kukamatwa kwa binti huyu na kuchukuliwa hatua stahiki.”
Dk Gwajima ametoa wito waliorekodi na kusambaza na wanaoijua familia hii watoe ushirikiano kwa kuwataja badala ya kuendelea kuisambaza.
“Nakemea watu wazima wanaowadhuru watoto kwa namna yoyote ile. Hatua kali zitachukuliwa wakibainiwa. Ahsante jamii mnaoendelea kuibua ukatili dhidi ya watoto. Tuendelee kuwa macho kuangaza kuibua ukatili dhidi ya watoto na kutoa taarifa,” ameandika Dk Gwajima.
Daktari wa binadamu, Paul Masua amesema kiafya mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya pombe tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
Baada ya kuzaliwa, bila kujali ni kwa kiwango gani atatumia, amesema pombe ina uwezo wa kumuathiri mtoto kama ilivyo kwa watu wazima, lakini kwa watoto madhara huwa zaidi.
“Ubongo wa mtoto haujakomaa, hivyo unapompa pombe unamweka katika hatari ya kupata magonjwa yanayoendana na ubongo, ikiwamo ugumu wa kujifunza shuleni, kuishi na watoto wenzake, kupata magonjwa ya akili hasa msongo wa mawazo na huweza kumfanya kupata ukichaa baadaye,” amesema.
Magonjwa mengine amesema ni ya moyo, presha na kisukari akieleza anapokuwa mkubwa hali huongezeka kulinganisha na mtoto ambaye hakunywa pombe.
“Hivyo, ili kumlinda mtoto na athari hizo, wazazi wanashauriwa kuhakikisha watoto hawatumii pombe kwa namna yoyote ikiwa ni baada ya kuzaliwa au anapokuwa tumboni kwa mama yake,” amesema.