RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA SOKO LA KISASA CHUINI, ATOA MAAGIZO SABA KUHUSU USIMAMIZI WAKE


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameuagiza uongozi wa Soko la Chuini kuhakikisha unadumisha usafi na nidhamu kwa kusimamia wafanyabiashara wote wafanye shughuli zao ndani ya maeneo rasmi yaliyotengwa.

Dkt. Mwinyi alitoa maagizo hayo leo, Septemba 4, 2025, alipofungua rasmi Kituo cha Mabasi na Soko la Kisasa la Chuini, lililopo Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi. Akipongeza mkandarasi na wasimamizi wa ujenzi, alisema soko hilo ni miongoni mwa miradi muhimu ya kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi alitoa maagizo saba kwa wasimamizi na mamlaka husika za masoko, ikiwemo kuimarisha usafi ndani na nje ya soko, kuzuia biashara holela nje ya soko na pembezoni mwa barabara, kutoza kodi nafuu, kufanya ukarabati wa mara kwa mara, na kuwaingiza wafanyabiashara mapema sokoni ili kuchangamsha shughuli za kibiashara. Aidha, alisisitiza kituo cha mabasi kuanza kazi mara moja na barabara inayozunguka eneo hilo kutengenezwa kwa kiwango cha lami haraka iwezekanavyo.

Vilevile, aliagiza taasisi za kifedha ziwe mstari wa mbele katika kuwasaidia wajasiriamali kwa mikopo nafuu ili kuchochea jitihada za kupunguza umasikini. Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga masoko ya kisasa katika maeneo ya Mombasa, Kibanda Maiti na maduka katika eneo la Malindi.

Akihitimisha, Rais Dkt. Mwinyi aliwakumbusha wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuendeleza mshikamano na amani wakati taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Soko la Kisasa la Chuini limejengwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, likiwa na maduka 98, maghala, maegesho ya magari na vyoo 26.