Tanzania Breweries PLC yakwama mahakamani ikizipinga TRAB, TRAT

Arusha. Mahakama ya Rufaa nchini imebariki uamuzi wa Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza Kuu la Rufaa za Kodi (TRAT) ya kukataa madai ya Kampuni ya Tanzania Breweries PLC kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya zaidi ya Sh6.532 bilioni.

Kampuni hiyo ambayo zamani ilijulikana kama Tanzania Breweries Limited inajishughulisha na utengenezaji, uuzaji na usambaji wa vileo na vileo visivyo na vyenye vilevi nchini Tanzania.

Kampuni hiyo ilikata rufaa katika Mahakama hiyo dhidi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

‎Mjibu TRA ilifanya ukaguzi katika biashara ya Tanzania Breweries PLC katika kipindi cha Aprili 2016 na Desemba 2017 na kufanya tathmini ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya zaidi ya Sh6. 532 bilioni, kati ya kiasi hicho deni halisi la kodi likiwa ni zaidi ya Sh4.888 bilioni  na Sh1.648 bilioni ikiwa ni riba.

‎‎Mrufani hakukubaliana na tathmini hiyo, hivyo Julai 29, 2019 aliwasilisha pingamizi, akidai kuwa TRA alikosea kutokuruhusu madai yake (Tanzania Breweries PLC) ya Kodi ya Ingizo (Input Tax) na hivyo kusababisha madai ya kodi ya VAT yasiyo sahihi.

Katika Mahakama ya Rufani, rufaa hiyo ilsikilizwa na jopo la majaji watatu – Dk Mary Levira, Dk Lilian Mashaka na Dk Deo Nangela, waliotoa uamuzi wao Septemba 4, 2025 na nakala ya uamuzi huo kupatikana kwenye tovuti ya Mahakama.

Rufaa hiyo ilitokana na hukumu na agizo la TRAT iliyotolewa Septemba 14, 2023, katika rufaa ya kodi namba 159 ya mwaka 2021.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Rufani iliunga mkono uamuzi wa TRAT na TRAB na kuikatalia kampuni hiyo madai ya kurejeshewa kodi hiyo na kutupilia mbali rufa yake.

Kampuni hiyo ilipinga tathmini hiyo na kuwasilisha pingamizi Julai 29, 2019 ambapo Desemba 27, 2019 Kamishna Mkuu wa TRA alisisitiza kuwa ankara za kodi za mrufani hazikukidhi kifungu cha 86 (1) (b) (v) cha Sheria ya VAT, 2014.

Mrufani alirejelea pingamizi lake Februari 4, 2020, na baadaye Kamishna Mkuu wa TRA alitoa uamuzi wake wa mwisho Machi 30, 2020 na kuthibitisha tathmini ya VAT kuwa sahihi.

Kwa kutoridhishwa na uamuzi huu, mrufani alikata rufaa yake TRAB akiwa na malalamiko mawili, kwamba uamuzi wa mjibu rufaa kudai ushuru wa ongezeko la thamani kwa mwaka 2016 hadi 2017 haukuwa sahihi kisheria.

Bodi hiyo ilisikiliza pande zote mbili na kutegemea matokeo yake katika kifungu cha 68 (1) kilichosomwa pamoja na kifungu cha 69 (2) cha Sheria ya VAT, kwamba kodi sahihi ni ankara inayozalishwa na kifaa cha kielektroniki cha fedha (EFD) na ndiyo ushahidi wa msingi wa kuunga mkono dai la kodi hiyo.

Bodi ilihitimisha kuwa hakuna ushahidi mwingine, isipokuwa ankara iliyotolewa na EFD inayoweza kuunga mkono madai ya kodi hiyo ya ingizo ambayo mtu anayetozwa kodi anastahili, chini ya kifungu cha 68 (1) cha Sheria ya VAT, 2014.

Bodi pia ilibaini kuwa ankara za kodi zilizozalishwa kwa mikono hazikuwa na ankara sahihi za kodi zilizotolewa na EFD, na kuhitimisha kwa kutupilia mbali rufaa hiyo.

Akiwa bado hajaridhika na uamuzi wa Bodi, mrufani alikata rufaa TRAT ambayo nayo ilikubali uamuzi wa Bodi ya TRAB.

Katika rufaa hiyo, Kampuni hiyo inapinga uamuzi wa Baraza ikiwa na sababu nne za rufaa ambazo ni Mahakama ya Rufani ya Mapato ya Kodi ilikosea kisheria kwa kushindwa kushikilia kwamba mjibu rufaa alikosea kukataa kodi ya ingizo ya mrufani kwa kupindi tajwa na kudai kodi ya VAT  inayodaiwa kuwa haijalipwa.

Nyingine ni kwamba mahakama hiyo ilikosea kisheria kushikilia kuwa haikuweza kuzingatia na kutathmini ushahidi uliotolewa na mrufani, ili kuunga mkono madai ya kodi ya pembejeo kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya VAT, 2014.

Sababu nyingine ni kuwa Mahakama ya Rufani ya Mapato ya Kodi ilikosea kisheria kushikilia kuwa mjibu rufaa alikuwa sahihi kuweka riba kwa mujibu wa kifungu cha 78 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo mrufani aliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Allan Kileo huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Consolatha Andrew.

Katika mawasilisho yao upande wa mrufani, ulidai kuwa Mahakama ilifanya makosa kisheria kwa kuthibitisha kukataa kwa mdaiwa kukataa madai ya kodi ya ingizo ya mrufani kwa kipindi tajwa juu.

Kuhusu suala la Ankara za kodi, ilidaiwa kuwa Mahakama ilihitimisha kimakosa kwamba ankara ya kodi ndiyo ushahidi pekee unaoruhusiwa kuunga mkono dai la kodi ya pembejeo na kumalizia kwa kuiomba mahakama kuruhusu rufaa hiyo.

Kwa upande wao, wajibu rufaa waliunga mkono uamuzi unaopingwa na kusema kuwa Bodi ilitafsiri kwa usahihi matakwa ya lazima ya Sheria ya VAT ya kudai deni la kodi ya pembejeo.

Ilielezwa kuwa, kifungu cha 86 (2) cha Sheria ya VAT ni kifungu mahususi na kisicho na utata ambacho kinakataza ankara zisizo na maelezo yanayotakiwa kutumika kuunga mkono madai ya kodi ya ingizo.

Walisisitiza kuwa haitoshi kuthibitisha kwamba kodi ya ingizo ililipwa kwa kiasi kikubwa; mlipakodi lazima aunge mkono dai na risiti ya fedha inayokubalika, kama ilivyoagizwa na sheria na kuwa riba chini ya kifungu cha 76 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ulikuwa halali.

Jaji Mashaka akisoma hukumu alianza kwa kueleza kuwa wamezingatia mawasilisho ya mawakili na kumbukumbu nzima ya rufaa, na kuwa wanadhani kwa sababu zilizotajwa, wanapaswa kuamua tafsiri sahihi ya vifungu vya 68, 69 na 86 vya Sheria ya VAT ya mwaka 2014.

Amesema kwa kuanzia, wataanza na sababu ya kwanza hadi ya tatu za rufaa ambazo zilijadiliwa kwa pamoja na mrufani, ambaye anamlalamikia mjibu rufaa kuwa alikataa kimakosa dai lake la kodi ya ingizo.

“Kupitia dondoo lililo hapo juu, linabainisha maelezo yote ambayo mrufani anapaswa kuwasilisha ili kuhalalisha dai lake, ushahidi ni ankara ya kodi inayotolewa na EFD ni lazima iwe na jina, anwani, nambari ya utambulisho ya mlipakodi na nambari ya usajili ya ongezeko la thamani ya mteja.

“Mrufani aliwasilisha risiti za mwongozo ambazo hazikuwa na jina la mrufani, TIN namba na namba ya usajili iliyoongezwa thamani, hivyo kinyume na kifungu cha 86 (1) (b) (v) cha Sheria ya VAT,”

Jaji Mashaka amesema mrufani katika hoja zake za kimaandishi alidai kuwa, mfumo wa EFD uliokuwa ukitumika wakati huo haukuwa na maeneo muhimu ya kujumuisha taarifa zinazohitajika, hivyo mrufani au wasambazaji wake wakashindwa kurekebisha au kuongeza maelezo yaliyokosekana.

Jaji Mashaka amesema wamebaini kuwa kodi ya VAT ilitathminiwa kwa usahihi na ukabakia bila kulipwa.

Jaji alihitimisha na kueleza kuwa kwa kanuni hiyo, maamuzi mbalimbali ya mahakama ya rufaa yaliyotajwa na upande wa mjibu rufaa yanayeleza msimamo sahihi wa sheria, wanakubali kwamba rufaa hiyo haina mashiko na wanaitupilia mbali pamoja na gharama.