Dar/Tanga. Chama cha Union Multiparty Democracy (UMD) kimeahidi kuwa endapo kitapewa dhamana ya kuongoza nchi, kitatekeleza mradi wa ‘mgodi’ wa machungwa katika Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, ili kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo kupitia kilimo cha zao hilo.
Aidha, chama hicho kimeahidi kuondoa adha ya upungufu wa maji kwa wananchi kwa kuwajengea visima katika kila mtaa wilayani humo.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Septemba 6, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Mwajuma Noti, wakati wa uzinduzi wa kampeni wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Mtumba, Muheza, jijini Tanga.
Kuhusu kilimo, Mwajuma amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais, Serikali yake itahakikisha maofisa ugani wanasimamia kwa ukaribu kilimo cha machungwa ili kitokee kwa mafanikio na kuwa chanzo cha maendeleo kwa wakulima wa Muheza.
“Kama mnavyofahamu Muheza ni hazina ya mchungwa na matunda, na Mwenyezi Mungu ameijalia kuwa na hazina hiyo na hakuna sehemu nyingine itakayopata ardhi ya kustawisha matunda hayo, hivyo tuna kila sababu ya kukiangalia kilimo hiki ili kiwanufaishe wana Muheza na Tanzania kwa ujumla,” amesema Mwajuma.
Kuhusu sekta ya maji, mgombea urais wa chama hicho amesema kuwa akipewa ridhaa, Serikali yake itatekeleza mpango wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa urahisi kwa kuchimbwa visima katika kila mtaa wilayani humo.
“Mkituchagua tutafanya uboreshaji wa miundombinu ya maji iliyopo na kuwajengea mingine mipya ili kuwaokoa wanawake ambao wanatembea umbali mrefu wa kutafuta maji,” amesema.
Kwa upande wa sekta ya afya, mgombea huyo amesema atahakikisha Serikali yake inaboresha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya, pamoja na kuboresha majengo na vifaa tiba vya hospitali, ili kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora.
Amesema pia kuwa Serikali yake itahakikisha wanaokwenda kujifungua wanapata huduma bure bila kutozwa gharama yoyote kwenye hospitalini zote za umma.
Aidha, Mwajuma amesema moja ya malengo makuu ya chama chake endapo kitapewa ridhaa ni kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumiwa kwa ufanisi ili kunufaisha wananchi wote, ikiwemo watoto tangu wakiwa wadogo.
Kwa mujibu wa mgombea huyo, endapo rasilimali hizo zitatumika vyema, zitasaidia pia kukuza hisia za utaifa miongoni mwa wananchi kwa kuwaona kuwa nchi inaendeshwa kwa manufaa ya kila mmoja.
“Mkituamini UMD ndani ya siku 100 tutahakikisha tunarekebisha mfumo wa elimu kwa kusimamia mfumo wa elimu ambao unakwenda kumkomboa mtoto anayekwenda shule kwa kuwekewa mazingira rafiki.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Moshi Kigundula, amesema salamu rasmi ya chama chao katika uchaguzi huu ni: “Uhuru, Haki na Amani.”
Akifafanua maana ya salamu hiyo, Kigundula amesema kuwa nchi imepata uhuru tangu mwaka 1960, lakini cha kushangaza ni kuona baadhi ya watu wanaonekana kuwa huru, huku wengine bado wakikumbwa na hali ya ukandamizwaji na ukosefu wa haki, hali aliyofananisha na utumwa mbaya zaidi kuliko ule wa kikoloni.
Kuhusu haki, amesisitiza kuwa mahali popote panapopatikana uhuru wa kweli, ndipo panapopatikana haki kwa wananchi.
“Katika hili la haki, sio wengine waonekane wanayo na wengine hawana kwa sababu tu ya umasikini wao na kutokuwa na vyeo au mamlaka,” amesema.
Kuhusu suala la amani, amesema pale ambapo kuna haki na uhuru wa kweli, amani lazima ipatikane. Ameomba amani hiyo iwe ya kweli, si ile ya kudhibitiana.
Naye Katibu wa Vijana wa chama hicho, Mohammed Mbonde, amewataka vijana nchini wasidanganyike au kuathiri amani ya taifa kwa ajili ya masilahi ya vyama vya siasa, kampeni au uchaguzi.
“Tafadhali vijana amani ni msingi wa Tanzania na si urithi wa Tanzania, kwa kuwa anayeichukulia kama urithi anaweza kuwa na viashiria vya kuivunja amani hiyo lakini anayeichukulia kama msingi wa nchi, atailinda kwa nguvu zote na popote alipo.
“Hivyo niwaase vijana na Watanzania wote nchini kuitunza amani hii kwani waasisi wetu wamepata taabu ya kuianzisha na kuilinda na tukiipoteza leo wa kuishika tena haitawezekana,” amesema Mbonde.