Walioingia kwenye mfumo wa Mfaransa Yanga watajwa!

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa mazoezi kambini Avic Town, Kigamboni chini ya kocha Romain Folz kikijiandaa na msimu mpya wa mashindano wa 2025-26, huku kocha huyo akiwa amelainishiwa mambo, licha ya kuwakosa zaidi ya wachezaji 10 walioitwa katika timu za taifa.

Yanga iliyoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu minne mfululizo, sambamba na Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano inajifua kwa ajili ya mechi ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi itakayofanyika Septemba 12, pia ikijiwinda na Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Hata hivyo, ikiwa kambini kwa sasa, kuna wachezaji 11 wa kikosi hicho wapo kwenye timu tofauti za taifa wakicheza mechi za kimataifa, jambo linaloonekana ni kama kumrahisishia kocha Folz mara nyota hao watakaporejea salama kwenye majukumu hao, kwani watakuwa wameiva kimashindano.

Ipo hivi. Yanga ni moja klabu za Ligi Kuu Bara zilizotoa wachezaji  wengi katika vikosi vya timu za taifa, ambapo wawili juzi walishuka uwanjani kusaidia timu zao katika mechi hizo za kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Wachezaji walioitwa katika timu za taifa ni; kipa Diarra Djigui ambaye juzi alikuwa langoni kuisaidia Mali kushinda mabao 3-0 dhidi ya Comoro, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya, Edmund John na Clement Mzize waliopo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambayo usiku wa jana ilikuwa uwanjani kuvaana na Congo Brazzaville.

Wengine ni, Lassine Kouma na Celestin Ecua waliopo Chad ambapo juzi walilazimisha sare ya 1-1 na Ghana, straika huyo mpya wa Yanga (Ecua) akichomoa bao dakika za jioni baada ya awali Jordan Ayew kuwatanguliza wageni kwa bao lililotokana na pasi na Mohamed Kudus katika dakika ya 17.

Viungo Balla Moussa Conte wa Gambia na Duke Abuya wa Kenya jioni ya jana walitarajiwa kuvaana katika pambano la Kundi F, wakiwa ni nyota wanaokamilisha idadi ya wachezaji 11 wa Yanga waliopo kwenye majukumu  ya kimataifa.

Kupata nafasi ya kutumika katika timu ya taifa, inawafanya wachezaji wao kuendelea kujiweka fiti kwa mashindano hata watakapoungana na wenzao kambini mara baada ya mechi za wiki ijayo, mashabiki wakiomba tu wasipate majeraha kipindi hiki klabu ikikabiliwa na mechi ngumu.

Yanga ukiacha mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Bandari Kenya itakayopigwa Septemba 12 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ina mechi dhidi ya Simba katika Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16, siku chache kabla ya kuifuata Wiliete Benguela ya Angola katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ikitoka hapo Yanga itakuwa na mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji itakayopigwa Septemba 24, ikiwa ni siku chache kabla ya kurudiana na Benguela, jijini Dar es Salaam ili kuamua klabu ya kwenda raundi ya pili ya michuano hiyo ya CAF.

Kwa namna ratiba ilivyo, wachezaji hao watashuka tena kwenye viwanja tofauti wakiwa na timu zao za taifa Sept 9, ambapo kwa wale wa Tanzania watamalizana na Niger kwenye Uwanja wa New Amaan kabla ya nyota hao kurejea kambini Yanga kuendelea na programu za Folz.

Kwa muda huo wa wachezaji kurejea nchini ina maana wachezaji watakuwa na saa chache kabla ya kushuka uwanjani kukabiliana na Bandari Kenya katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi na siku chache kabla ya pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Hii ikiwa na maana kwamba kama wachezaji hao watarudi wakiwa kamili gado, basi haitakuwa kazi kubwa kwa kocha Folz kumalizia maandalizi ya kuanza msimu mpya, japo kuna wachezaji ambao hajawahi kufanya nao kazi kabisa tangu atue Jangwani akiwamo Dickson Job, Bacca, Tshabalala, Mzize na Mudathir waliokuwa na Stars katika fainali za CHAN 2024 zilizomalizika mwezi uliopita.

Winga mpya Edmund John amefanya naye kazi kwa muda mchache tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Singida Black Stars kabla ya kuitwa Stars kwa ajili ya mechi hizo mbili za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Nyota anayeweza kuchelewa kuungana na wenzao mapema mazoezini baada ya mechi hizo za kimataifa ni Conte ambaye timu ya taifa ya Gambia itacheza usiku wa saa 4:00 ya Septemba 9 dhidi ya Burundi kabla ya kupanda ndege kurudi Tanzania.

Wachezaji wengine kati ya hao 11, mechi zao zinapigwa Septemba 8 na mapema jioni siku ya mwisho yaani Septemba 9 wakiwamo saba wa Taifa Stars watakaokuwa hapo tu, visiwani Zanzibar.