Chato. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM), ikiahidi miradi mbalimbali Mkoa wa Geita, wananchi wa Katoro wametaka Halmashauri ya Geita Vijijini igawanywe ili kuwapunguzia adha ya kutembelea zaidi ya kilomita 80 kufuata huduma.
Novemba 4, 2019, Halmashauri ya Geita ilihamia Kata ya Nzera iliyopo Jimbo la Geita Vijijini. Wananchi wanataka igawanywe iwe Halmashauri ya Geita na Halmashauri ya Katoro.
Wagombea ubunge na udiwani wamemweleza Dk Nchimbi kwamba, Katoro kibiashara unafanana na soko la Kariakoo la jijini Dar es Salaam na wafanyabiashara na wananchi wanasota kuifikia Halmashauri iliyoko Nzera.
Kilio hicho cha wananchi kimetolewa na wagombea ubunge na udiwani katika mkutano wa kampeni za mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi uliofanyikia eneo la Katoro na Bwanga mkoani Geita.
Dk Nchimbi amebainisha kile ambacho watakifanya miaka mitano ijayo baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa Mkoa wa Geita ni kuiboresha Hospitali ya Kanda ya Chato na vitongoji vyote kufikiwa na umeme na kuimarisha sekta ya mifugo kwa kuongeza majosho

Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi leo Septemba 6, 2025 akiwa Kagera. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo wataongeza kasi ya utoaji leseni kwa wachimbaji wadogo, ujenzi wa hospitali mpya, zahanati na shule za msingi na sekondari.
“Miaka mitano ijayo tutaimarisha sekta ya madini, kasi ya utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo itaongezwa. Tutaongeza idadi ya hospitali kutoka saba zilizopo sasa hadu 10, tutaongeza idadi ya vituo vya afya kutoka 44 hadi 61, tutaongeza idadi ya zahanati mpya kutoka 215 za sasa hadi 271.
“Ujenzi wa shule za msingi kutoka 757 hadi 770, ujenzi wa madarasa kutoka 12,650 ya sasa hadi 22,716, tutaongeza mtandao wa majisafi na salama, kuimarisha ruzuku ya mbolea na mbegu ili kuleta tija katika kilimo cha pamba na kuimarisha skimu za umwagiliaji,” amesema Dk Nchimbi.
Mgombea mwenza huyo amesema, katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itakayoundwa na CCM chini ya Rais Samia itahakikisha mkoani Geita uimarishawa mifugo unazingatiwa kwa kuboresha majosho, pamoja na kupeleka umeme katika vitongoji vyote.
Dk Nchimbi akizungumza na wananchi na wanachama wa Wilaya ya Chato yenye majimbo mawili ya Chato Kusini na Chato Kaskazini eneo la Bwanga amesema miaka mitano ijayo wataendelea kuiboresha Hospitali ya Kanda ya Chato ili itoe huduma bora zaidi.
Kilio cha Halmashauri kugawanywa
Aliyekuwa wa kwanza kutoa kilio hicho ni mgombea ubunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ambaye amesema:”Hapa ni Katoro na ni Kariakoo ya Kanda ya Ziwa, sasa hivi tunakutama na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) tunazungumza na tunamaliza salama.”
Musukuma amesema walikuwa na tatizo la maji Katoro ambalo kwa sasa halipo.
Huku akishangiliwa, Musukuma amesema:”Sisi Wasukuma tumebarikiwa sana kuzaa, ukikuta mwenye watoto wachache ni 15 na mimi mwenyewe ninayo 18, lakini Halmashauri imekaa vibaya, kutoka hapa kwenda Halmashauri ni kilomita zaidi ya 80.”
Amemwomba Dk Nchimbi baada kuingia madarakani, Halmashauri igawanywe ziwe mbili ili kusogeza zaidi huduma za jamii na majengo ya kuanzia yapo.
Musukuma amesema tayari kuna hospitali mbili za wilaya iliyopo Katoro na nyingine Nzera:”Tunaomba mtutazame kwa jicho la pekee. Tunaomba katika siku 100 mtugawie tuwe na halmashauri mbili moja iwe hapa ya Katoro kwani kutoka hapa Katoro hadi Nzera ni kilomita zaidi ya 80.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na mgombea ubunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko amesema:”
Hapa Katoro, kama alivyosema Musukuma, hawa hawana maneno mengi wanajishughulisha kupata kipato. Wanachohitaji wao ni maendeleo na yamekuwa makao makuu ya biashara hapa Geita. Unaweza usipate kitu Chato au Kadete utaipata hapa.”
“Sisi kazi yetu kwa watu wa Katoro ni kuja kuwakumbusha kwamba wako wagombea wa aina mbili. Wanakuja kusema walichokifanya, kama maji yamekuja, umeme umekuja, lakini wako wengine wanatamani kufanya.”
Dk Nchimbi alipomwita, mgombea udiwani Lutede, Jumanne Misungwi naye amegusia hilo la halmashauri akisema hawana shaka Oktoba 29 kutakuwa na ushindi wa kishindo lakini hapa:”Wanazaliana kwa wingi kama alivyopsema Musukuma na ninaomba tuongeze halmashauri ili tupunguze adha ya kwenda kule Nzera.”
Hoja hiyo imezungumzwa pia na mgombea ubunge wa Katoro, Kija Ntemi ambaye alipopewa fursa ya kuwasalimia wapiga kura wake amesema kazi kubwa imefanyika ya kuwaletea maendeleo wananchi.
“Ili kuleta maendeleo Jimbo la Katoro, mheshimiwa mgombea mwenza, tunaomba kuwa na halmashauri yetu, wafanyabiashara hawa wanatembea zaidi ya Kilomita 80.
“Hapa tuna benki za kutosha. TRA wapo hapa, wafanyabiashara wanachohitaji ni kuwasogezea tu huduma. Tunaomba sana Dk Nchimbi hili tulifanyie kazi,” amesema Ntemi.
Baada ya Ntemi kumaliza kuzungumza, Dk Nchimbi akasema:”
Mmemsikiliza mbunge, mna bonge la mtetezi na anaweza kusemea matatizo yenu, anaishi na sisi, anatujua.”
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotolea kwenye mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu