Musoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka watu wanaohoji sababu za kumsifu mwenyekiti wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kuacha malalamiko na badala yake wajikite katika kufanya mambo yenye tija kwa maendeleo ya wananchi, ili nao wapate sifa.
Wasira amesema si vibaya kiongozi kusifiwa pale anapotekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na kwamba badala ya kubeza juhudi zinazofanywa na Rais Samia, ni vyema watu hao wakajitathmini na kufanya kazi kwa bidii ili wachangie maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Samia amefanikisha utekelezaji wa mambo makubwa ya maendeleo, ikiwemo kuboresha huduma za kijamii kama afya, maji, elimu na sekta nyingine muhimu.
Aidha, ameongeza kuwa CCM bado ina dhamira ya kuendelea kutekeleza miradi mikubwa zaidi kwa manufaa ya wananchi na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo, Septemba 6, 2025, mjini Musoma, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Jimbo la Musoma Mjini, Wasira amesema lengo la chama hicho ni kuendelea kushika dola ili kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
Wasira amesema ndio maana chama kimeandaa ilani bora ya uchaguzi inayojikita katika kushughulikia mahitaji halisi na changamoto zote zinazowakabili wananchi, kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli na endelevu.
“Sasa wanalalamika nini wakati hawana chochote walichokifanya, sisi lazima tumsifie wa kwetu kwa sababu amefanya mengi sana na tunayaona, sasa wewe unalalamika wakati hata zahanati hujajenga, fanya maendeleo na wewe usifiwe kwa sasa tuko na mama Samia,” amesema.
Amesema miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kufanywa na chama hicho katika Mkoa wa Mara kwa ujumla ni pamoja ujenzi wa vituo vya afya vipya 18, zahanati mpya 37 pamoja na huku sekta ya elimu na zingine zikitarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa.
Kuhusu uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa mkoa kwa ujumla, Wasira amesema yapo mengi yanayotarajiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Musoma sambamba na kuimarishwa kwa sekta ya kilimo kwa kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili wananchi waachane na kilimo cha kutegemea mvua.
“Kwa kweli mambo ni mengi nikianza kutaja kila kitu hapa basi tutalala Mukendo, itoshe kusema tuna mipango mizuri sana na nyie, tutakwenda kufufua viwanda na kila kitu ili mradi uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa mkoa uimarike,” amesema.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Benedict Magiri amesema wana CCM ndani ya wilaya hiyo wana mshikamno kwa asilimia 89 baada ya kuvunjwa kwa makundi yaliyotokana na mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
“Tumepita kwenye kata zote 16 za Manispaa ili tusemane, tuzungumze na tuwekane sawa lengo kuu likiwa ni kuvunja makundi ili wana CCM tuimbe wimbo mmoja wa Chama cha Mapinduzi,” amesema.
Amesema anaamini kwa vikao hivyo walivyofanya wanachama wa chama hicho sasa hivi wameshikamana na kwa pamoja wanatafuta kura za chama kuanzia urais hadi udiwani.
Mgombea ubunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji amewaomba wakazi wa jimbo hilo kukipigia kura Chama cha Mapinduzi huku akisema changamoto zote za wakazi wa jimbo hilo zinakwenda kupatiwa ufumbuzi.
“Changamoto kubwa ya Musoma ni ajira na uchumi niwaombe nyie mniachie hilo jukumu nyie kazi yenu ni kumchagua Mgore, mama Samia na madiwani wote wa CCM halafu muone tutakayofanya,” amesema
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Iddi Mkowa amesema chama hicho kinaamini katika utawala wenye kuzingatia usawa wa kijinsia kwa vitendo na kwamba katika kuhakikisha hilo linafanikwa wagombea ubunge katika majimbo manne kati ya kumi yaliyopo mkoani humo ni wanawake.
Ameyataja majimbo hayo na wagombea wake kuwa ni pamoja na Mgore Miraji (Musoma Mjini), Mary Daniel (Serengeti), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Esther Bulaya (Bunda Mjini).
Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Gaudensia Kabaka amesema hii ni mara ya kwanza kwa chama hicho kusimamisha wagombea wengi wanawake kwa nafasi ya jimbo mkoani Mara.
“Hii haikuja kwa bahati mbaya, wote tunajua Mkoa wa Mara ulikuwa na sifa gani kuhusu wanawake lakini kazi imefanyika na kwa sasa tunaona matunda, niipongeze kamati kuu kwa kazi nzuri haikuwa rahisi lakini hakika wameweza,” amesema.
Mgombea ubunge Tarime Mjini, Esther Matiko amesema Mkoa wa Mara umeongoza nchini kwa kuteuwa idadi kubwa ya wagombea wanawake ambao ni sawa na asilimia 40 na kwamba katika historia ya mkoa huo haijawahi kutokea, na hivyo watashirikiana na wabunge wengine na madiwani wote kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa kwa asilimia 100.
“Mara huko nyuma tulikuwa tukitambulika kama mkoa ambao hauthamini wanawake hasa kwenye masuala ya uongozi, lakini CCM chini ya Rais Samia imeidhihirishia dunia kuwa Mara tunaweza, kilichobaki ni kupiga kura ili tufanye kwa vitendo,” amesema Matiko.
Aliyekuwa mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo amesema hana shida na maamuzi yaliyofanywa na chama chake kwa maelezo kuwa chama hicho ni kikubwa zaidi ya mtu binafsi.
“Wanaosema nina kundi, sio kweli kwanza mimi sikuwa mgombea, lakini pia najivunia kufanya kazi na marais wanne na muda wote tumeleta maendeleo yanayoonekana kwa macho,” amesema.