Mwanza. Chama cha UPDP kimesema kitakapoingia madarakani, yeyote atakayehusika kuchelewesha mafao ya wastaafu ataadhibiwa kwa kifungo na kupoteza kazi, bila kujali cheo chake.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Mwanza Septemba 5, 2025 na mgombea urais wa chama hicho, Twalib Kadege, wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Alisema suala la wastaafu kusubiri kwa muda mrefu mafao yao ni kero kubwa inayohitaji mabadiliko ya haraka ya kisheria.
Kadege alieleza kuwa tarehe ya kustaafu inajulikana kwa kila mwajiri, hivyo taarifa za wastaafu lazima ziwasilishwe mapema ofisi ya muhasibu mkuu wa taasisi husika ili maandalizi ya malipo yafanyike mapema.
“Hata kama ni waziri au kiongozi wa ngazi ya juu kiasi gani, adhabu hii itamuhusu na atapoteza kazi moja kwa moja. Tarehe ya mtumishi kustaafu inajulikana kwa kila mwajiri, hivyo taarifa za mstaafu mtarajiwa zipelekwe ofisi ya muhasibu mkuu wa taasisi, iwe ya umma au ya binafsi, siku kadhaa kabla ya kustaafu ili mafao yake ayaandaliwe mapema,”alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa kila mstaafu apewe barua inayoonyesha mafao anayostahili na tarehe ya malipo.
Aliahidi pia kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kuongeza mishahara mara mbili ili kuondoa tamaa ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhilifu.
Kadege alisema watumishi watawekewa utaratibu wa mafunzo ya maadili ya mara kwa mara, huku mfumo wa kuwafuatilia uwajibikaji wao ukianzishwa.
“Atakayebainika kuwa mzembe kazini atafikishwa mahakamani na kupoteza mafao yake yote. Haiwezekani daktari au muuguzi akaona mgonjwa anateseka halafu akakaa kimya,” alisema.
Kadege alionya zaidi kuhusu rushwa, akibainisha kuwa katika utawala wake ni bora mtu akameza chuma kuliko kutumia fedha ya umma kinyume cha sheria.
Aidha, aliahidi kuwa vyombo vya habari vitapewa uhuru na uwezo wa kufika popote nchini na kuripoti miradi inayodorora kwa sababu ya ufisadi ili Serikali ichukue hatua.
Mgombea udiwani Kata ya Kirumba, Otieno Odull, alisema kipaumbele chake ni upatikanaji wa maji safi na salama akidai kwa sasa wananchi wanapata huduma hiyo mara mbili pekee kwa wiki, jambo linalo sababisha usumbufu mkubwa.
Aliahidi pia kurudisha daraja la chuma lililokuwapo katika eneo la Mwaloni, kando ya Ziwa Victoria, ambalo limeondolewa kwa madai ya ukarabati bila wananchi kupewa taarifa za maendeleo yake.
“Matokeo yake watu wanalazimika kutembea ndani ya maji kufuata mitumbwi, hali inayohatarisha usalama wao, huku ushuru ukiendelea kutozwa,” alisema.
Mkaazi wa Igoma, Julieth Masila alisema ana imani na ahadi zinazotolewa na wagombea wa vyama vyote, lakini akasisitiza matarajio yake ni kuona huduma za afya zinapatikana kwa urahisi kwa kila Mtanzania.