Iringa. Utalii wa puto ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa umeonekana kupata umaarufu kwa wageni kutoka mataifa ya nje huku wazawa wakiendelea kuwa wachache.
Akizungumza na Mwananchi Digital Septemba 5, 2025 katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo mkoani Iringa, Meneja wa kituo cha balloon safari Ruaha, Vincent Kavaya amesema kuwa hadi sasa asilimia 25 ya watalii wanatumia utalii wa puto huku asilimia 0.5 tu wakiwa ni wazawa.
Kavaya amefafanua na kueleza kwamba utalii wa puto hufanyika alfajiri na hubeba watu 12 kwa safari moja hivyo njia hiyo huruhusu kuona wanyama kwa ukaribu zaidi kwa muda mfupi eneo kubwa tofauti na utalii wa kutumia magari.
”Zao la utalii wa puto ni burudani kwa watalii kwani mara baada ya kushuka katika puto hupata muda wa kunywa mvinyo wa sherehe na kupata chai ya pamoja,” amesema Kavaya.
”Kuhusu gharama za utalii kwa njia ya puto kwa mtalii wa ndani ni Sh990,000 na wa mtalii kutoka nje ya nchi ni Sh 1,360,000, ” amesema Kavaya.
Pia, Kavaya ameeleza kwamba licha ya utalii wa puto kuonekana ni ya gharama bado ni utalii wa kipekee na wenye manufaa kwa hifadhi kwani hauharibu mazingira kama magari.
Mtaalamu wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Mariam Jilala amesema utalii wa puto ni bora kwani hauna kelele, hautumii mafuta na hauharibu njia za wanyama hivyo kusaidia uhifadhi wa ikolojia.
”Tukumbuke kuwa maeneo ya hifadhi yanapaswa kulindwa kwa umakini mkubwa hivyo utalii wa puto ni kielelezo tosha cha utunzaji wa mazingira, ” amesema Mariam.
Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Amina Salum, amesema kwa wanaoingia hifadhini, watoto hulipa Sh 2,360 tu na watu wazima Sh 5,900.
Nao baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa wameeleza kuwa wangependa kushiriki utalii wa puto katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha lakini kikwazo ni gharama kubwa ya huduma hiyo.
Wananchi hao wamesema kuwa licha ya kuvutiwa na namna utalii huo unavyofanyika kwa upekee, bado haulingani na kipato cha wananchi wa kawaida.
Katika hatua nyingine Wananchi hao wameeleza kuwa wanahofia usalama wao kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna puto hilo la anga linavyofanya kazi huku wakikiri kuwa wamekuwa wakiona huduma hiyo kupitia vyombo vya habari au mitandaoni tu.
”Kwakweli ningetamani sana kupanda hilo puto, maana ni kitu cha tofauti, lakini gharama ni kubwa mno kwa sisi watu wa kawaida. Halafu pia nahofia mambo ya hewani, kama likidondoka je?,” amesema Maria Nkwama mkazi wa Kihesa.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, baadhi ya Watalii waliowahi kutumia utalii huo wameeleza hisia zao.
John Peter, raia wa Marekani, amesema,
“Sijawahi kuona wanyama wa karibu namna hii. Upepo na utulivu wa puto unafanya kila kitu kiwe cha kuvutia,”
Neema Masangula, mkazi wa Iringa amesema
“Ningependa kujaribu lakini hiyo bei ni kubwa sana kwetu watu wa kawaida,” amesema.
Aidha ili kuchochea utalii wa puto kuweza kukua zaidi, Wadau wa utalii kutoka mkoani Iringa wanashauri kampeni za elimu kwa umma zifanyike pamoja na kuwashirikisha wanafunzi na vikundi vya vijana ili kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye utalii huo ambao unatajwa kusaidia kuhifadhi mazingira kwa njia endelevu.