Zitto azindua kampeni akiahidi kurejesha heshima ya Kigoma

Kigoma/Dar. Uwanja wa Mwami Ruyagwa, mjini Kigoma umegeuka bahari ya zambarau, umati uliovaa vazi la rangi hiyo ulipofika kushuhudia uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Zitto, kiongozi mstaafu wa chama hicho amesema leo Septemba 6, 2025 kuwa safari yake ya kisiasa iliyoanza mwaka 2015 na kukwama 2020 sasa itaendelea kwa nguvu mpya.

Amesema dhamira yake kuu ni kurejesha heshima ya Jimbo la Kigoma Mjini na Mkoa wa Kigoma, akibainisha kuwa miradi mingi imedorora kutokana na kukosa usimamizi makini wa wabunge.


Ametoa mfano wa mitaa ya Bungu akisema imechakaa, jambo linalohitaji mbunge makini kuisimamia Serikali kuhakikisha huduma za kijamii zinaboresha maisha ya wananchi.

Zitto pia amezungumzia changamoto za ulinzi wa Bandari ya Kigoma, akidai imekabidhiwa kwa wawekezaji wa Kichina.

“Bandari ni mali ya wananchi wa Kigoma na haiwezi kuchezewa. Nitumeni bungeni ili nilinde masilahi ya mali zetu,” amesema.

Zitto akizungumzia masuala ya uhamiaji amehoji wananchi: “Nani wa kwanza kupigiwa simu mtu akikamatwa kwa tuhuma za uhamiaji haramu?”

Wananchi walimjibu kwa sauti: “Wewe” akatumia majibu hayo kujenga hoja ya namna amekuwa akiwatetea, akiwaomba wamrudishe bungeni aendelee kuwatetea.

Akizungumzia nafasi ya Kigoma katika ramani ya kitaifa na kikanda, amesema mkoa huo ni lango muhimu la kibiashara linalopaswa kunufaisha wananchi wake. Amewaomba wananchi wasichezee kura zao, bali wachague viongozi makini kutoka ACT-Wazalendo watakaosimamia fursa za kiuchumi na kijamii za mkoa huo.

Zitto amesisitiza mshikamano wa wananchi bila kujali vyama, akibainisha kuwa maendeleo hayahitaji mgawanyiko wa itikadi za vyama vya siasa.

“Tuachane na mgawanyiko wa vyama, sisi sote tunahitajiana, Kigoma haitachezewa tena wala watu wake hawatanyanyaswa,” amesema.

Aliyekuwa mpinzani wake ndani ya chama hicho katika jimbo hilo, Abdul Nondo, amepanda jukwaani akimuunga mkono Zitto kwa kuhimiza wananchi kumchagua mgombea huyo akimwelezea kuwa: “Kiongozi makini mwenye uwezo wa kujenga hoja na kusikilizwa bungeni.”


Mwenyekiti wa ngome ya wanawake Jimbo la Kigoma Mjini, Stela Shirima amewaomba wanawake kukipigia kura chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao ili kutatua changamoto zinazowakabili wanawake, ikiwamo mikopo maarufu kwa jina la kausha damu.

Kabla ya uzinduzi huo, wafuasi wa ACT-Wazalendo wakiongozwa na viongozi wa mkoa na Nondo walifanya maandamano ya hamasa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi katika maandamano hayo Zitto amewashukuru na kuahidi kuwatumikia akisema yeye ndiye awezaye kuwatetea katika changamoto zinazowakabili.

“Jasho hili nalichukulia kwa uzito mkubwa na ndiyo maana mmetembea zaidi ya saa tatu, hakuna ninaloweza kulifanya kwa usahihi mkubwa ni kuwatumikia wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji,” amesema.


Katika uzinduzi huo wagombea ubunge wa chama hicho wa majimbo ya Kigoma Kaskazini, Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini na Muhambwe pamoja na wagombea udiwani 19 katika jimbo hilo walihudhuria.