Zoran amvuta Mavambo Libya | Mwanaspoti

BAADA ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Debora Mavambo kuachana na timu hiyo aliyoitumikia kwa msimu mmoja aliyojiunga nayo Julai 6, 2024, kwa sasa mchezaji huyo anakaribia kujiunga na Asswehly ya Libya kwa mkataba wa miaka miwili.

Mavambo aliyejiunga na Simba akitokea Mutondo Stars ya Zambia na kufunga bao moja tu katika Ligi Kuu Bara huku akitabiriwa makubwa, alishindwa kuwika ndani ya kikosi hicho na sasa anakaribia kujiunga na Asswehly inayofundishwa na Kocha Zoran Maki.

Zoran mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno, aliifundisha Simba aliyotua Juni 28, 2022 akichukua nafasi ya Pablo Franco raia wa Hispania, ingawa aliondoka Septemba 6, 2022 baada ya kufikia makubaliano ya kusitishiana mkataba.

Awali, ilielezwa Mavambo angejiunga na Singida Black Stars ambayo ilionyesha nia ya kumhitaji baada tu ya kuachana na Simba, lakini dili hilo lilishindwa kukamilika na kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine nje ya Tanzania.

Vyanzo mbalimbali kutoka Libya vinaeleza Mavambo ni pendekezo la Zoran ambaye amewaomba viongozi kukamilisha dili la nyota huyo anayeamini anaweza kukisaidia hicho kilichoanzishwa Mei 11, 1944.

Mmoja wa viongozi wa Singida Black Stars aliliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli walifanya mawasiliano ya moja kwa moja na mchezaji huyo kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo, lakini dili halikufanikiwa ndipo walipochukua uamuzi wa kutafuta nyota mwingine.

“Mazungumzo yalikuwepo na tuliyafanya baada ya kuachana na Simba. Suala la maslahi halikuwa tatizo kwetu kwa sababu kila kitu kilikwenda vizuri isipokuwa mchezaji mwenyewe hakuwa tayari kuicheza ligi ya Tanzania,” kilisema chanzo hicho.