APR, KMC zajiweka pazuri CECAFA Kagame Cup

MIAMBA ya soka la Rwanda, APR na vijana wa Kinondoni, KMC zimejiweka pazuri kutuinga nusu fainali kutokana na kushinda mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Kagame 2025 inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Jana Jumamosi, KMC ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bumamuru ya Burundi, likifungwa na Erick Mwijage dakika ya 20 ya mchezo.

Bao hilo lilitosha kuwapa wakazi wa Kinondoni pointi tatu muhimu na kuendeleza matumaini yao ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Ushindi huo ulikuwa wa pili, KMC ilianza mashindano hayo kwa kuichapa Mlandege kwa mabao 3-2, ilihali APR iliendeleza ubabe wake kwa kuwafunga mabingwa wa Zanzibar pia kwa mabao 2-0.

Katika mechi ya kwanza ya mashindano hayo, APR iliifunga Bumamuru 2-0, hivyo kuifanya mechi baina yao inayopigwa leo kuwa ni mtego kwa kila mmoja kwani timu itakayopoteza itaiacha mwenzake kwenda nusu fainali na yenyewe kusikilia matokeo ya mwsho ya makundi mengine.

Lakini zikitoka sare zitafikisha pointi saba na kusikilizia matokeo ya mechi za Kundi A lenye Singida BS na Coffee zenye uwezo wa kufikisha pointi kama hizo na hivyo kuangaliwa tofauti na mabao ili kuungana pamoja kucheza nusu fainali itakayochezwa Ijumaa wiki hii.

Kwa sasa kila timu ina pointi sita, hivyo moja ikishinda itafikisha tisa na itakayopoteza itasaliwa na sita, lakini Kundi A linalocheza leo, Singida BS na Coffee kila moja ina uwezo wa kufikisha pointi saba, jambo linaloweza kuikwamisha timu itakayopoteza kutoka Kundi hilo la B.

Akiongelea ushindi wao dhidi ya Bumamuru, Mwijage aliyefunga bao pekee kwa KMC, alisema anajivunia mchango wake kwa timu na alifurahishwa na kuona juhudi zake zikitoa matunda.

“Nina furaha kubwa kuipa timu yangu ushindi muhimu. Bao hili lina maana sana kwetu katika hatua hii ya mashindano,” alisema Mwijage, huku kocha wa KMC, Marcio Maximo, alisifu nidhamu na ari ya wachezaji wake, licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa Bumamuru.

“Wameonyesha utulivu mkubwa na kujituma. Ni jambo la kutia moyo kuona vijana wakipambana katika kiwango hiki,” alisema Maximo.

Aliongeza ushiriki wao katika Kagame Cup utakuwa maandalizi bora kwa msimu wa Ligi Kuu Bara 2025/26. “Mashindano haya ni sehemu ya maandalizi yetu. Tunahitaji kuwa na mechi za ushindani wa juu ili kujiweka tayari kwa changamoto za ligi,” alibainisha kocha huyo.