Bado Watatu – 21 | Mwanaspoti

BAADA ya kumtoa shaka yake tuliendelea kuongea mawili matatu, tukacheka kidogo kisha tukaagana.

Niliendelea na shughuli zangu za kupika hadi saa sita mchana nikawa nimeshaivisha wali kwa nyama. Hicho ndicho chakula alichokuwa anakipenda mume wangu. Alikuwa akipenda wali kwa nyama kama Mhindi!

Ilipofika saa saba Sufiani akarudi nyumbani, nikapakua chakula tukala. Baada ya kula tulizungumza kidogo kisha tukaenda kulala.

Tuliamka saa kumi tukaenda kuoga. Tulipomaliza tulirudi chumbani tukavaa. Wakati tunavaa nikamwambia mume wangu kuwa nitatoka niende saluni kwangu kwa vile sikuwahi kufika tangu asubuhi, na yeye akaniambia pia anataka kutoka.

Kama mwanamke sikuacha wivu, nikamuuliza:

“Mh! Kila ninapokwenda unataka upajue?”

“Nina njia nyingi. Nataka nikutane na Shefa. Pia nataka tukamuone yule mtu mwenye mzigo wake unaokwenda Nairobi.”

“Wewe ukishakutana na Shefa hurudi mapema na utakuja umelewa!”

“Hapana. Leo sitakunywa. Si utaniona nitakaporudi.”

“Labda nikupeleke wewe saluni halafu nilitumie. Nikimaliza mizunguko yangu nikupitie.”

Baada ya muda wa kama nusu saa hivi Sufiani aliniacha kwenye saluni yangu akaondoka. Wakati nikiwa hapo saluni shoga yangu Raisa akanipigia simu.

Tukapiga stori kwa karibu robo saa. Mwisho akaniiambia.

“Kuna kitu nataka nikwambie. Mumeo yupo?”

“Hayupo, ametoka. Mimi pia sipo nyumbani?”

“Nataka tuonane, nina mzungumzo mafupi na wewe”

“Hebu nidokeze kidogo”

“Ah! Huyu rafiki yake mumeo ananisumbua sana!”

“Ananiambia eti unamuumiza sana”

“Ninamuumiza kwa lipi?”

“Mh…! Eti ambiwa anakuzimikia sana…halali!”

“Makubwa! Shefa si shemeji yangu, rafiki wa mume wangu!”

“Ndiyo hivyo. Siku zote anatafuta njia ya kuzungumza na wewe haipati, ndiyo akaona anitume mimi”

“Ambiwa! Lakini sikiliza Rukia hii habari iwe ni siri yetu mimi na wewe na huyo Shefa. Tafadhali usimwambie mumeo wala mtu yeyote. Usije ukanisaliti”

“Nikusaliti kwa ajili gani shoga yangu kwani kutakana si jambo la kawaida tu. Hiyari ni yangu mimi kukubali au kuukataa”

“Unajua ananisumbua sana. Usimkatae. Muonjeshe japo siku moja, roho yake itulie”

Kwa ile mara ya kwanza, yale mazungumzo sikuyapenda nikamwambia.

“Raisa tutakuja kuzngumza, hapa niko kazini”

“Nimekudokeza tu. Lakini enedelea kufikiria na wewe mwenyewe”

“Usijali. Tutakuja kuzungumza”

Hapo ndipo nilipopata picha, kumbe yule bwana akija nyumbani ana lake jambo lakini alikuwa anashindwa kulisema. Akaona aende akamwambie Raisa.

Nikajiuliza amenipenda mimi kwa uzuri gani zaidi ya ule alio nao mke wake?

Sufiani alinifuata saa tatu usiku. Tulikuwa tunafunga saluni akanisubiri kwenye gari. Baada ya kufunga saluni nikaenda kujipakia tukaondoka.

Muda wote nilikuwa nikiuwaza ule ujumbe niliopewa na Raisa kutoka kwa Shefa, rafiki wa mume wangu.

Ujumbe huo ulikuwa umeteka hisia zangu zote kwa sababu tangu nilipoolewa na Sufiani sikuwa na tabia ya kuchepuka nje na sikuwaza kwamba itakuja siku nitachepuka.

Nilikuwa najiuliza Shefa aliwaza nini kwangu mpaka akafikiria anitongoze kupitia kwa Raisa?

Kwa vile nilikuwa na mawazo hayo sikuwa na mzumngumzo na mume wangu. Tulibaki kimya mpaka tulipofika nyumbani. Tukaegesha gari na kuingia ndani.

Asubuhi ya siku iliyofuta Sufiani akaenda zake Dar. Alipoondoka tu nyumbani nikampigia simu Raisa.

Baada ya kusalimiana naye nikamuuliza.

“Ulisema utakuja tuzungumze, utakuja saa ngapi?”

“Kwani mumeo hayupo?”

“Ameondoka sasa hivi”

“Amekwenda Dar, kazini kwake”

“Namalizia kunywa chai ninakuja”

Nikakata simu. Ikapita kama saa moja hivi Raisa akaja nyumbani. Niliposikia mlango unabishwa nikajua ni yeye, nikaenda kuufungua.

“Karibu shoga” nikamkaribisha huku nikiufunga mlango.

Raisa alikaa kwenye kochi na mimi nikaenda kukaa kwenye kochi jingine.

“Shoga jana umenishitua sana” nikamwambia.

“Si yale maneno uliyonieleza jana”

“Sasa umemfikiriaje?”

“Wewe uliniambia tutakuja kuzungumza ndiyo nilikuwa nasubiri tuzungumze”

“Yule mwanaume ananisumbua sana, yaani ananiambia Raisa nakutegemea wewe. Hii leo asubuhi pia amenipigia simu”

“Ameniuliza kama nimeshazungumza na wewe. Nikamwambia nimekudokeza tu lakini hatujazungumza kikamilifu”

“Hivi unafikiri mimi naweza kutembea na Shefa?” nikamuuliza Raisa.

“Yule si rafiki wa mume wangu, si afadhali angekuwa mtu baki”

“Kwani akiwa rafiki wa mume wako ana nini?”

“Si vizuri. Mume wangu akija akijua unafikiri itakuwaje?”

“Hawezi kujua. Mume wako kila siku yuko kwenye safari zake, atajuaje?”

“Yaani wewe Raisa unakubaliana na jambo hilo?”

“Sasa tatizo liko wapi. Yule anajidai ana visenti vinamsumbua. Mimi natataka umle vile visenti vyake”

“Lakini si ana mke wake?”

“Babu kakupenda wewe!”

“Mke wake atanielewaje jamani?”

“Hakuelewi chochote. Kwani unadhani yule mwanamke hana mabwana wa nje? Anao vizuri”

“Mh! Acha kwanza nifikiri”

“Wewe hata kama unafikiria, anza kumla!”

“Raisa mbona una pupa. Hivyo vihela vyake havinibabaishi. Acha kwanza nifikirie”

“Haya wewe fikiria lakini akiniuliza nitamwambia nimeshakwambia”

“lakini chondechonde Rukia, usiniangushe. Uje umuonjeshe japo siku moja”

“Nimuonjeshe imekuwa ni karanga!”

Nilipomuuliza hivyo tukacheka.

Mpaka Raisa anaondoka pale nyumbani saa tano nilikuwa bado nikiwaza kuhusu yale maneno yake. Nikajiambia nitahitaji muda mrefu wa kutafakari na kujishauri.

Zikapita siku tatu hivi. Raisa alikuwa akinipigia simu karibu kila siku kuniulizia nilichoamua. Jibu langu llilikuwa “Bado nafikiria”

“Nije naye nyumbani kwako?” Kuna siku akaniuliza hivyo.

“Kwani mume wako si yuko safarini au amerudi”

“Hajarudi bado lakini usije naye. Njoo wewe tu tuzungumze”

“Kwanini nisije naye?”

“Yule anakuja mume wangu akiwepo”

“Nina maana mje mzungumze”

“Acha tuendelee hivi hivi tu, kama kuna mazungumzo yatapitia kwako lakini ukweli hadi sasa hivi sijaamua chochote”

“Mmhh…! Raisa akatoa mguno mzito kabla ya kuniambia.

“Sawa mwaya lakini bado nakutegemea”

Kwa kweli wazo lile la kuwa na mahusiano na Shefa halikuafikiana na akili yangu ila nilipanga kwamba kuna siku tamwambia Raisa aachane na wazo hilo.

Baada ya kusafiri kwa wiki mbili Sufiani alirudi. Alikuja mchana. Akafika nyumbani kisha akatoka. Kwa kujua mume wangu yuko sikwenda kazini kwangu. Saa kumi jioni akaja nyumbani akiwa amefuatana na Shefa.

Kusema kweli nilishituka na sikuweza kutazamana na Shefa machoni. Nilikuwa nikimuona aibu ingawa yeye alijichangansha kunisemesha.

Wakati tumekaa sebuleni watu watatu tukizungumza, Shefa alikuwa akichezea simu yake, ghafla nikaona sms mbili zimeingia katika simu yangu.

Nikafungua meseji ya kwanza na kukuta maneno yaliyosema.

“Nimepata ujumbe wako”

Namba iliyotuma meseji ilikuwa namba ya Shefa.

Meseji ya pili ilikuwa ni ya pesa. Alikuwa amenitumia shilingi laki mbili”

Nikamtupia jicho Shefa mara moja tu kisha nikafuta zile meseji haraka. Moyo wangu ulikuwa ukienda mbio.

Kulikuwa na siku Malikia wa mipasho alikuwa akifanya onesho lake katika ukumbi mmoja maarufu hapo jijini, tukaenda na kurudi usiku wa manane. Kwa vile tulitumia usafiri wa teksi, nilishushwa mimi kwanza nyumbani kwangu kisha teksi ikaenda kumshusha Raisa nyumbani kwake.

Asubuhi yake Shefa mwenyewe akanipigia simu tukazungumza sana na siku hiyo ndpo nilipomuahidi aje nyumbani usiku kwa vile Sufiani hakuwepo.

Siku ile Raisa hakunipigia simu na mimi sikumpigia. Sikutaka ajue kuwa nilikuwa na ahadi na Shefa japokuwa yeye ndiye aliyeufanya mpango huo.

Ilipofika saa tatu usiku Shefa alinipigia simu akaniambia kuwa anataka kuja nyumbani.

“Subiri. Unajua watu wa hapa nyumbani hawajalala bado. Kwani huwezi kuja kwenye saa sita hivi?”

“Basi njoo muda huo. Nitaacha mlango wazi, ukija unaingia tu”